Dec 06, 2016 03:37 UTC
  • Jumuiya za kutetea haki za binadamu zatahadharisha kuhusu hali ya wanawake Nigeria

Jumuia mbalimbali za kutetea haki za binadamu zimetahadharisha kuhusu hali mbaya ya wanawake nchini Nigeria.

Jumuiya hizo likiwemo shirika la Amnesty International zimetangaza kuwa, wanawake na wasichana wa Nigeria waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram wakati mwingine wanatumiwa katika mashambulizi ya kujilipua kwa mabomu.

Ripoti hiyo imesema kuwa, baadhi ya wanawake wa maeneo yenye idadi kubwa ya Waislamu ya kaskazini mashariki mwa Nigeria wanajiunga na kundi la Boko Haram kwa matarajio ya kupata maisha bora kutokana na umaskini wa kupindukia, ubaguzi wa kijinsia na mfumo dume uliokita katika maeneo hayo.

Wasichana na wanawake waliotekwa nyara na Boko Haram, Nigeria

Ripoti ya Amnesty International imesisitiza kuwa, wanawake wengi wamekuwa wakimbizi kutokana na mapigano yanayoendelea katika maeneo hayo na wanalazimika kuuza miili yao kwa ajili ya kupata chakula.

Kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limetangaza ushirika wake na kundi la Daesh, limeua maelfu ya watu na kulazimisha wengine karibu milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi katika nchi za Nigeria, Cameroon, Chad na Niger tangu lilipoanza uasi katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria.     

Tags