Miili sita yapatikana mtoni Mkoa wa Pwani, nchini Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21010-miili_sita_yapatikana_mtoni_mkoa_wa_pwani_nchini_tanzania
Maiti sita ambazo hazijatambulika zimekutwa zikielea katika Mto Ruvu eneo la Bagamoyo, Mkoa wa Pwani nchini Tanzaia, zikiwa zimehifadhiwa kwenye mifuko ya plastiki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2016 06:07 UTC
  • Miili sita yapatikana mtoni Mkoa wa Pwani, nchini Tanzania

Maiti sita ambazo hazijatambulika zimekutwa zikielea katika Mto Ruvu eneo la Bagamoyo, Mkoa wa Pwani nchini Tanzaia, zikiwa zimehifadhiwa kwenye mifuko ya plastiki.

Gazeti la serikali la Habari Leo la Tanzania limemnukuu Diwani wa Kata ya Makurunge, Paul Kabile ambaye amesema maiti hizo ambazo ni za jinsia ya kiume ziligunduliwa na wavuvi na zimeharibika kiasi cha kutotambulika.

Amesema maiti hizo ziligunduliwa Disemba 6, majira ya alfajiri kwenye Kitongoji cha Kitopeni wilayani Bagamoyo, ambako wavuvi  waligundua miili hiyo wakati wakiendelea na shughuli zao za uvuvi kwenye mto huo.

Amesema “Maiti hizo kila moja ilikuwa imehifadhiwa kwenye kiroba huku zikiwa zimewekewa mawe na mifuko hiyo ikiwa imeshonwa juu kama vile yamehifadhiwa mahindi au mchele na kwamba wavuvi hao baada ya kuziona maiti hizo walizizika kutokana na kuharibika sana na kushindwa kuzipeleka hospitali kuzihifadhi.

Diwani wa Kata ya Makurunge, Paul Kabile ameongeza kuwa maiti tano ziligunduliwa juzi alfajiri na nyingine moja iligundulika jana.

Mwandishi wa Habari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, Hassan Mtengevu alithibitisha kutokea tukio hilo, na kueleza kuwa wanafanya uchunguzi kwa kushirikiana na daktari ili kufahamu watu hao walikufa kwenye mazingira gani.