Kutamba Khalifa Haftar huko Libya
Katika hali ambayo jeshi la Libya linaloongozwa na Kamanda Khalifa Haftar linajiandaa kukabiliana na watu ambao limewataja kuwa ni makundi yenye misimamo mikali huko Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo, kamanda wa oparesheni ya kuukomboa mji wa Sirte mashariki mwa Tripoli amemuarifisha mtawala wa kijeshi wa mji huo.
Jenerali Bashir al Qadhi Kamanda wa chumba cha oparesheni ya kuukomboa mji wa Sirte amemuarifisha Jenerali Ahmad Abu Shahma kuwa mtawala wa kijeshi wa mji huo huko mashariki mwa Tripoli. Mji wa Sirte una umuhimu kwa kuzingatia kuwa, kwa upande mmoja ni eneo alikotokea Kanali Muammar Gaddafi na aghalabu ya wakazi wake ni wafuasi wa utawala uliopita; na kwa upande wa pili, ni mji unaotambulika kuwa kituo muhimu cha magaidi wa Daesh nchiniLibya.
Jeshi la Libya chini ya uongozi wa Kamanda Khalifa Haftar lilielekeza juhudi zake kubwa kwa ajili ya kuukomboa mji wa Sirte kutoka mikononi mwa magaidi wa kundi la Daesh na hatimaye likaweza kuukomboa mji huo. Hata kama kukombolewa mji wa Sirte ambao ulikuwa ukishikiliwa na magaidi wa Daesh kwa kiasi kikubwa kunahesabiwa kuwa sawa na kufikia ukomo harakati za magaidi hao huko Libya au kwa uchache huko Sirte, lakini kukombolewa mji huo hakumaanishi kumalizika hali ya mchafukoge katika mji huo. Kwa msingi huo, Kamanda wa chumba cha oparesheni ya kuukomboa mji wa Sirte amemteuwa mtawala wa kijeshi wa mji huo ambaye atachukua hatua za kuzuia kuibuka tena machafuko katika mji huo. Kwa kuainishwa mtawala huyo wa kijeshi katika mji wa Sirte, ni wazi kuwa Khalifa Haftar ambaye ni kamanda wa jeshi la taifa la Libya anajiandaa kuendesha vita na wale aliowataja kuwa ni watu wenye misimamo ya kuchupa mipaka huko Tripoli. Ahmad al Mismari Msemaji wa jeshi la taifa la Libya ametangaza kuwa jeshi hilo hivi sasa linaudhibiti mji mkuu Tripoli ambao liliupoteza miaka miwili iliyopita. Msemaji wa jeshi la taifa la Libya ameyasema hayo katika hali ambayo Jenerali Khalifa Haftar yupo karibu na serikali yenye makao yake mashariki mwa Libya huku akikabiliana na serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj. Wakati huo huo serikali ya Fayez al Sarraj ambayo ilipendekezwa kuasisiwa kufuatia makubaliano ya Sakhirat Disemba mwaka jana inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa na madola ya Magharibi. Khalifa Haftar anajiandaa kupambana na makundi aliyoyaita kuwa yenye misimamo mikali huko Tripoli; huku serikali ya Fayez al Sarraj ikiwa bado haijajiimarisha kitaifa. Katika uga huo, kutamba huko kwa Jenerali Khalifa Haftar kwa mara nyingine tena kunaweza kuipeleka pambizoni serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na kuzidisha pia migogoro ya kisiasa na kiusalama nchini humo.
Jambo lililo na umuhimu zaidi ni hili kwamba hakuna kiongozi yoyote wa kijeshi wa Libya si Khalifa Haftar wala Ahmed al Mismari ambaye ameweka wazi wanaowakusudia wanaposema wanakenga kukabiliana na makundi yenye misimamo mikali huko Tripoli? Hii ni katika hali ambayo Ahmed al Mismari msemaji wa wa jeshi la kitaifa la Libya amebainisha kuwa Tripoli ni shabaha ya kiistratejia ya oparesheni maalumu za kijeshi za kuwaangamiza magaidi katika awamu ijayo na kwamba vikosi vya jeshi hilo vimeajiandaa kutekeleza opareshen hiyo ya kuukomboa mji mkuu huo.