FAO: Watu milioni 12 Afrika Mashariki wanahitajia msaada wa chakula
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limetahadharisha kuwa, watu milioni 12 katika kanda ya Afrika Mashariki wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na njaa.
Taarifa ya FAO imesema kuwa, watu milioni 5 wanahitajia msaada wa dharura wa chakula nchini Somalia huku Waethiopia milioni 5.6 wakisakamwa na baa la njaa.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limebainisha kuwa, Kenya imetumbukia katika orodha ya nchi zisizo na usalama wa chakula na kwamba watu milioni 1.3 katika nchi hiyo wanahitajia msaada wa chakula. Limesema maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo hususan Turkana, Marsabit, Wajir na Mandera yataendelea kusakamwa na njaa hadi kufikia katikati ya mwaka ujao 2017.

Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limeongeza kuwa, maeneo ya mashariki mwa Tanzania na kusini mashariki mwa Uganda pia yanashuhudia ukame kutokana na mvua kunyesha chini ya kiwango cha wastani mwaka huu.
Mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, FAO ilisema itadhamini mbegu, mbolea, na huduma zinazohitajiwa na wakulima katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame barani Afrika.
Wataalamu wa FAO wanafanya jitihada za kuhakikisha wanawasaidia wakulima karibu milioni 23 wa maeneo yaliyokumbwa na mgogoro wa chakula barani humo hadi kufikia mwaka 2018. Wataalamu hao wanahitaji bajeti ya dola milioni 109 kwa ajili ya kutekeleza mpango huo.