Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Gambia akimbia nchi baada ya kutishiwa maisha
(last modified Wed, 04 Jan 2017 07:10:25 GMT )
Jan 04, 2017 07:10 UTC
  • Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Gambia akimbia nchi baada ya kutishiwa maisha

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Gambia amekimbia nchi akihofiwa usalama wake.

Familia na watu wa karibu na Alieu Momar Njai, wamesema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Gambia amekimbia nchi baada ya kutishiwa maisha kwa kumtangaza Adama Barrow mshindi wa uchaguzi wa Disemba Mosi mwaka uliomalizika 2016. 

Hata hivyo wamesema Momar Njai hakutoa maelezo zaidi kuhusu ni nani aliyemtishia maisha na ni wapi amekimbilia.

Yahya Jammeh, rais aliyeshindwa katika uchaguzi wa Disemba Mosi, 2017

Mgogoro huo wa kisiasa nchini Gambia umesababisha hali ya taharuki huku vyombo vya usalama vikifunga vituo vya redio vya Teranga FM na Hilltop Radio. Hata hivyo serikali haijatoa taarifa yoyote kuhuhusiana na tukio hilo ingawaje inaarifiwa kuwa huenda vilifungwa kwa kumkashifu Yahya Jammeh kwa kukataa kukabidhi madaraka.

Rais Yahya Jammeh ambaye amekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 22 alishindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka jana na kukubali matokeo yaliyompa ushindi hasimu wake Adama Barrow. Hata hivyo siku chache baadaye aliibuka na kutilia shaka matokeo hayo sanjari na kukataa kuondoka madarakani.

Adama Barrow, mfanyabiashara aliyetangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais Gambia

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) imetishia kutuma vikosi vya kieneo nchini Gambia, iwapo Rais Yahya Jammeh atakataa kukabidhi madaraka wakati muda wake utakapiomalizika rasmi Januari 19 mwaka huu.

Tags