Viongozi wa Kiafrika wasisitiza juu ya kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23545-viongozi_wa_kiafrika_wasisitiza_juu_ya_kupambana_na_ugaidi
Viongozi wa nchi 30 za Kiafrika walioshiriki katika mkutano wa Afrika na Ufaransa huko Bamako mji mkuu wa Mali wamesisitiza juu ya kuweko vita vya kweli dhidi ya ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 15, 2017 11:13 UTC
  • Viongozi wa Kiafrika wasisitiza juu ya kupambana na ugaidi

Viongozi wa nchi 30 za Kiafrika walioshiriki katika mkutano wa Afrika na Ufaransa huko Bamako mji mkuu wa Mali wamesisitiza juu ya kuweko vita vya kweli dhidi ya ugaidi.

Rais Ibrahim Boubacar Keita wa mali ambaye nchi yake mara hii ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo wa Afrika na Ufaransa uliomalizika jana amesema kuwa, pamoja na mambo mengine washiriki wa mkutano huo wamejadili mbinu na mikakati ya kupambana na tishio la ugaidi na kuongezwa nafasi ya kisiasa na kijamii ya wananchi katika maamuzi makubwa ya bara hilo.

Marais wa Mali na Ufaransa walioongoza mkutano wa 27 wa Afrika na Ufaransa mjini Bamako

Rais wa Mali amesema kuwa, mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo wa 27 wa Afrika na Ufaransa yalikuwa chanya na kusisitiza kwamba, ustawi wa kiuchumi na vijana kupewa nafasi zaidi katika masuala mbalimbali ni mambo ambayo yanaweza kuongeza kasi ya ustawi na maendeleo ya nchi za bara la Afrika.

Mkutano wa 27 wa Afrika na Ufaransa mara hii umefanyika katika hali ambayo nchi nyingi za bara la Afrika zinakabiliwa na changamoto tofauti zikiwemo za hitilafu za ndani, vita na mapigano, njaa na ukame, uingiliaji wa kigeni na kutwishwa siasa za kikoloni. Katika hali ya hivi sasa wananchi wa nchi kama Sudan Kusini, Burundi, Gambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanakabiliwa na migogoro tofauti ya kisiasa.