Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusiana na ukame nchini Somalia
(last modified Wed, 18 Jan 2017 16:39:07 GMT )
Jan 18, 2017 16:39 UTC
  • Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusiana na ukame nchini Somalia

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusiana na kuongezeka matatizo ya Somalia kutokana na ukame unaoikabili nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Peter de Clercq, Mratibu wa Umoja wa Mataifa Katika Masuala ya Kibinadamu nchini Somalia ametangaza kuwa, hali ya kibinadamu kwa mamilioni ya wananchi wa nchi hiyo ni ya kutia wasiwasi ikiwa ni natija ya kushadidi ukame nchini humo.

Amesema, takribani watoto laki tatu na elfu ishirini wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na hali mbaya ya lishe duni na kwamba 50 elfu kati yao wana hatari ya kupoteza maisha endapo hawatapatiwa msaada wa haraka. 

Hivi karibuni Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa, uhaba wa maji katika nchi za Somalia na Ethiopia umesababisha karibu watoto milioni tatu kukumbwa na hatari ya utapiamlo, huku karibu raia milioni tano wa Somalia wakihitaji misaada ya chakula.

Hali mbaya iliyosababishwa na ukame

Taathira hasi za El-Nino  sambamba na ukame na mafuriko katika nchi za Somalia na Ethiopia zimeyaweka hatarini maisha ya watu wengi wa nchi hizo.

Mbali na majanga hayo ya kimaumbile, Somalia inakabiliwa na harakati za kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab ambalo limekuwa likifanya mashambulizi ya kigaidi kila leo.

Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, nusu ya wananchi wa Somalia hawana uwezo kamili wa kupata chakula. Aidha ufikishaji misaada ya chakula kwa wahitaji limekuwa jambo gumu kutokana na ukosefu wa usalama.