Waasi Sudan Kusini waituhumu Misri kuwa imeshambulia ngome zao
Waasi wa Sudan Kusini wameituhumu Misri kuwa imeshambulia kwa mabomu maeneo na ngome zao na kutahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea vita vya kieneo.
Taarifa iliyotolewa na waasi wa kundi la makamu wa zamani wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar imesema kuwa, kikosi cha Jeshi la Anga cha Misri kimedodosha mabomu na mada za milipuko katika vituo na maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa SPLA-AO karibu na kijiji cha Kaka kilichoko maeneo ya kaskazini mwa Sudan Kusini.
Taarifa hiyo pia imeituhumu serikali ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kuwa inataka kupanua zaidi vita vya ndani nchini humo.
Taarifa ya waasi wanaomfuata Machar imesisitiza kuwa, ushiriki wa Misri katika vita vya ndani ya Sudan Kusini ni kielelezo cha wazi kwamba, serikali ya Juba inachochea vita vya kikanda na kuielekeza Sudan Kusini katika vita vya kieneo.
Madai hayo yamekanushwa na serikali ya Sudan Kusini na vilevile Misri. Msemaji wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Ateny Wek Ateny amesema kuwa madai hayo hayana msingi wowote.
Vilevile msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, Ahmed Abu Zeid amekanusha madai kuwa, ndege za kivita za nchi hiyo zimeshambulia ngome za waasi nchini Sudan Kusini na kuongeza kuwa, Misri haiingilii masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kwamba alifanya jaribio la kumuondoa madarakani kupitia njia ya mapinduzi.