Waasi Sudan Kusini wadai Misri imewashambulia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24721-waasi_sudan_kusini_wadai_misri_imewashambulia
Waasi Sudan Kusini wameituhumu Misri kuwa imetekeelza hujuma za angani katika ngome zao huku wakuu wa Cairo wakikanusha kufanya hivyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2017 03:56 UTC
  • Waasi Sudan Kusini wadai Misri imewashambulia

Waasi Sudan Kusini wameituhumu Misri kuwa imetekeelza hujuma za angani katika ngome zao huku wakuu wa Cairo wakikanusha kufanya hivyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa upande mmoja hasimu Sudan Kusini kuituhumu Misri kuwa inaingilia kijeshi mgogoro wa nchi hiyo ambao ni baina ya jeshi la Rais Salva Kiir na waasi wanaomtii makamu wake wa zamani  Riek Machar.

Taarifa iliyotolewa na kundi la waasi lijulikanalo kama SPLA-IO imesema ndege za kivita za Misri Ijumaa zilidondosha zaidi ya mabomu tisa katika kijiji cha Kaka jimbo la Upper Nile.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri Ahmed Abu Zeid alikanusha kuwepo mashambulio hayo na kusisitiza kuwa, "Misri haingilii mambo ya ndani ya nchi zingine."

Naye Msemaji wa Rais wa Sudan Kusini Ateny Wek Ateny pia amekanusha kuwa Misri imetekeleza hujuma nchini humo na kutaja madai hayo kuwa ya kipuuzi.

Rais Kiir wa Sudan Kusini (kushoto) na kiongozi wa waasi Reik Machar

Wakati huo huo Ateny amesema kwamba mazungumzo ya kitaifa yanayokuja yatakuwa wazi kwa makundi yote ya upinzani ikiwa ni pamoja na kiongozi wa waasi aliyeko uhamishoni Riek Machar.

Mwezi Desemba mwaka jana, Rais Kiir aliidhinisha mazungumzo ya kitaifa ili kumaliza mapigano yaliyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu nchini humo na kuleta ahueni na maridhiano kati ya pande mbalimbali.