UN yatahadharisha kuhusu machafuko Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24975-un_yatahadharisha_kuhusu_machafuko_sudan_kusini
Umoja wa Mataifa umevitahadharisha vikosi vya jeshi la serikali na wapinzani huko Sudan Kusini kuhusu kuendeleza hali ya machafuko nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2017 21:54 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu machafuko Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umevitahadharisha vikosi vya jeshi la serikali na wapinzani huko Sudan Kusini kuhusu kuendeleza hali ya machafuko nchini humo.

Adama Dieng Mshauri Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kuzuia mauaji ya kimbari ameitahadharisha serikali ya Juba kuhusu uwezekano wa kushtadi machafuko nchini Sudan Kusini na kueleza kuwa, Rais Salva Kiir wa nchi hiyo anapaswa kufanya jitihada za kufufua mazungumzo kati yake na kambi ya upinzani.

Adama Dieng, Mshauri Maalumu wa Katibu Mkuu wa UN katika kuzuia mauaji ya kimbari 

Adama Dieng ameongeza kuwa, mchakato wa mazungumzo ya kitaifa ambao ulitazamiwa kuanza Sudan Kusini unapaswa kujumuisha machaguo ya kisiasa yenye maana kwa ajili ya viongozi wa upinzani na si kwa watu kama Riek Machar, makamu wa zamani wa Rais wa nchi hiyo ambaye hashiriki katika mazungumzo hayo.

Riek Machar mwezi Julai mwaka jana aliukimbia mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba baada ya kupamba moto hitilafu kati yake na Rais Salva Kiir.

Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko na mapigano kati ya wafuasi wa Rais Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar tangu mwaka 2013. Vita vya ndani nchini humo vimewalazimisha raia karibu milioni tatu kuwa wakimbizi katika nchi jirani na maelfu ya wengine kuuawa. 

Wakimbizi wa Sudan Kusini waliopata hifadhi nchini Uganda