Nchi za Afrika Magharibi kuunda kikosi cha kukabiliana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2509-nchi_za_afrika_magharibi_kuunda_kikosi_cha_kukabiliana_na_ugaidi
Mawaziri wa ulinzi wa eneo la Sahel huko magharibi mwa Afrika wameazimia kuunda kikosi cha jeshi cha pamoja cha radiamali ya haraka ili kukabiliana na ongozeko la hatari ya makundi ya kigaidi ya al Qaeda na Daesh katika eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 06, 2016 02:40 UTC
  • Nchi za Afrika Magharibi kuunda kikosi cha kukabiliana na ugaidi

Mawaziri wa ulinzi wa eneo la Sahel huko magharibi mwa Afrika wameazimia kuunda kikosi cha jeshi cha pamoja cha radiamali ya haraka ili kukabiliana na ongozeko la hatari ya makundi ya kigaidi ya al Qaeda na Daesh katika eneo hilo.

Kutokana na kuwepo jangwa kubwa na mipaka isiyodhibitiwa kikamilifu, eneo la Sahel limegeuka na kuwa uwanja wa kueneza ugaidi katika eneo hilo ambalo ni kati ya maeneo masikini zaidi duniani.

Katika mkutano huo uliofanyika mji mkuu wa Chad, N’Djamena, mawaziri wa ulinzi wa Chad, Niger, Burkina Faso, Mali na Mauritania waliahidi kuunda kikosi maalumu cha kukabiliana kwa kasi na hujuma na vitisho vya makundi ya kigaidi.

Nchi hizo ambalo zinajulikana kama G5 Sahel zimesema kutakuwa na makundi kadhaa ya askari 100 waliopewa mafunzo ya hali ya juu na wenye uwezo wa kutumwa haraka katika maeneo yenye magaidi sugu.

Katibu Mkuu wa G5 Sahel, Najim Elhadj Mohamed, amesema askari hao wanatumia mbinu kama zilizokuwa zikitumiwa na jeshi la Uhispania kukabiliana na kundi la waasi ETA waliokuwa wakipigania kujitenga eneo la Basque. Amesema askari hao wa nchi za Sahel wamepata mafunzo kutoka Ufaransa na Uhispania.

Nchi za eneo hilo zimekuwa zikikumba na hujuma za kigaidi katika miezi ya hivi karibuni kutoka kundi la kigaidi la al Qaeda katika eneo la Maghrib AQIM na kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limetangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi la Daesh.