UN: Wakimbizi waliotoweka Sudan Kusini hatima yao haijulikani
Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi ulionao kutokana na kutokuweko taarifa za kutosha kuhusiana na hali ya wakimbizi waliotoweka huko katika nchi ya Sudan Kusini.
David Shearer, Mkuu wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS ametangaza kuwa, kukosekana taarifa za kutosha kuhusiana na wakimbizi wa Sudan Kusini wapatao elfu 20 limekuwa tatizo kubwa kwa serikali ya nchi hiyo pamoja na askari wa kofia buluu wa umoja huo.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa wanafanya juhudi za kuingia katika kijiji cha Wau Shilluk kilichoko katika jimbo la Upper Nile kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini, lakini makundi ya waasi na vikosi vya serikali vimekuwa vikiwazuia askari hao wa Umoja wa Mataifa.
David Shearer amesema kuwa, ameshangazwa na vizuizi hivyo ilhali lengo la askari wa Umoja wa Mataifa la kwenda katika kijiji hicho ni kutaka kufahamu hatima ya wakimbizi hao.
Machafuko ya ndani Sudan Kusini yalianza mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kwamba amehusika na jaribio la kutaka kupindua serikali yake.
Hitilafu za kisiasa na kikabila zinatajwa kuwa sababu kuu za mapigano na mivutano ya mara kwa mara kati ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka na hasimu wake, Machar anayetoka kabila la Nuer.