Mkuu wa Mahakama za Kijeshi Sudan Kusini ajiuzulu, aishutumu serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25320-mkuu_wa_mahakama_za_kijeshi_sudan_kusini_ajiuzulu_aishutumu_serikali
Mkuu wa Mahakama za Kijeshi nchini Sudan Kusini, Kanali Khalid Ono Loki amejiuzulu na kueleza kwamba uingiliaji unaofanywa kutoka ngazi za juu umesababisha kutowezekana kuwachukulia hatua za kuwaadhibu askari wanaotuhumiwa kufanya ubakaji na mauaji wakati wa vita vya ndani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 18, 2017 12:51 UTC
  • Mkuu wa Mahakama za Kijeshi Sudan Kusini ajiuzulu, aishutumu serikali

Mkuu wa Mahakama za Kijeshi nchini Sudan Kusini, Kanali Khalid Ono Loki amejiuzulu na kueleza kwamba uingiliaji unaofanywa kutoka ngazi za juu umesababisha kutowezekana kuwachukulia hatua za kuwaadhibu askari wanaotuhumiwa kufanya ubakaji na mauaji wakati wa vita vya ndani nchini humo.

Katika barua yake ya kujiuzulu kwa Mkuu wa Majeshi, Loki amesema askari wamekuwa wakitenda jinai bila ya kuwa na hofu ya kuadhibiwa, hususan maafisa kutoka kabila la Dinka ambalo ni la Rais Salva Kiir wa nchi hiyo pamoja na Mkuu wake wa Majeshi. Aidha amemkosoa vikali Mkuu huyo wa Majeshi kwa kueleza kwamba: "Umetoa amri ya raia kutiwa nguvuni na kuwekwa kwenye jela za kijeshi kinyume na taratibu sahihi za kisheria… Siwezi tena kuendelea kufanya kazi na taasisi kama hiyo fisadi, yenye ukabila na isiyo na maadili".

Hata hivyo msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Brigedia Jenerali Lul Ruai Koang amedai kuwa Kanali Khalid Ono Loki alikuwa amejiuzulu tangu mwaka jana lakini suala hilo lilikuwa halijatangazwa hadharani.

Luteni Jenerali Thomas Cirillo Swaka

Kanali Ono Loki ni kiongozi wa tatu wa ngazi za juu wa serikali ya Sudan Kusini kujiuzulu ndani ya kipindi cha wiki moja. Jumamosi iliyopita, Naibu Mkuu wa Majeshi anayehusika na masuala ya kilojistiki Luteni Jenerali Thomas Cirillo Swaka alijiuzulu kulalamikia vitendo vya unyanyasaji vikiwemo vya udhalilishaji wa kingono unaofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya raia na kile alichokiita kuongezeka upendeleo wa kikabila jeshini.

Hapo jana pia Waziri wa Leba Luteni Jenerali Gabriel Duop Nam alitangaza kujiuzulu na kusema kuwa sasa ataunga mkono harakati zinazofanywa na waasi wanaomuunga mkono Riek Machar, Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo…/