Kiir awaachia huru majenerali wa jeshi na wafungwa wa kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26226-kiir_awaachia_huru_majenerali_wa_jeshi_na_wafungwa_wa_kisiasa
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir amewaachia huru makamanda waandamizi wa jeshi la nchi hiyo na kuahidi kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa katika siku zijazo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2017 03:17 UTC
  • Kiir awaachia huru majenerali wa jeshi na wafungwa wa kisiasa

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir amewaachia huru makamanda waandamizi wa jeshi la nchi hiyo na kuahidi kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa katika siku zijazo.

Akihutubia umati wa watu katika mji mkuu Juba jana Ijumaa, Rais Kiir alisema: "Sijakuja hapa kufanya siasa, nimekuja hapa kuwaachia huru Jenerali Elias Waya and Jenerali Andrea Dominic."

Jenerali Waya ambaye alikuwa Gavana wa Jimbo la Wau, kaskazini magharibi mwa nchi alikamatwa pamoja na naibu wake Jenerali Dominic Juni mwaka jana 2016, na tangu wakati huo wamekuwa wakizuiliwa katika jela ya kijeshi mjini Juba. Serikali ya Salva Kiir haikutoa maelezo yoyote kuhusu sababu za kukamatwa kwa maafisa hao wa ngazi za juu wa serikali yake.

Rais Kiir (Kushoto) na aliyekuwa Makamu wake Riek Machar

Rais Kiir ameahidi kwamba ataachia huru wafungwa wengine wa kisiasa leo Jumamosi na wengine kesho Jumapili, hatua inayojiri masaa machache baada ya nchi hiyo kuadhimisha Siku ya Maombi ya Taifa hapo jana.

Hivi karibuni Kiir alitangaza kuwa, taifa hilo changa zaidi barani Afrika litafanya uchaguzi mwaka ujao 2018, baada ya kumalizika kipindi hiki cha mpito.

Alitoa wito kwa wapinzani akiwemo hasimu wake wa kisiasa, Riek Machar, kukomesha mapigano na kurejea nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya zoezi hilo la kidemokrasia linalotazamiwa kufungua ukurasa mpya katika siasa za nchi hiyo.