Unicef na Wfp zatoa msaada wa chakula kwa Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26984-unicef_na_wfp_zatoa_msaada_wa_chakula_kwa_sudan_kusini
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa pamoja zimegawa misaada mbalimbali kwa raia 145,000 wa Sudan Kuisni wakiwemo watoto elfu 33 walio na umri wa chini ya miaka mitano.
(last modified 2025-11-19T08:00:07+00:00 )
Mar 29, 2017 02:56 UTC
  • Unicef na Wfp zatoa msaada wa chakula kwa Sudan Kusini

Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa pamoja zimegawa misaada mbalimbali kwa raia 145,000 wa Sudan Kuisni wakiwemo watoto elfu 33 walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Jeremy Hopkins Mwakilishi wa Unicef huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini jana alibainisha kuwa timu 13 za huduma za kibinadamu zimeelekea katika mkoa wa Unity ili kuwasaidia wenyeji wa mkoa huo waliokumbwa na baa la njaa. Hopkins ameongeza kuwa watoto wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 250,000 wana  utapiamlo huko Sudan Kusini.Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) amesema athari kubwa za mgogoro wa chakula ulioiathiri Sudan Kusini umelipelekea shirika hilo kuanza haraka oparesheni za kibinadamu ili kuzuia vifo vya watoto.

Wakimbizi wa Sudan Kusini wakiwa katika moja ya kambi nchini mwao

Amesema watoto zaidi ya 7500 walio na umri chini ya miaka mitano ambao wana utapiamlo wamefanyiwa uchunguzi huku watoto wapatao elfu 25 wakipatiwa chanjo dhidi ya polio na surua. 

Taarifa ya Unicef imeongeza kuwa, imesajili majina ya watoto zaidi ya 40 ambao hawana wazazi walezi. Watoto hao wamesajiliwa ili kuweza kufahamu mahala zilipo familia zao. Serikali ya Sudan Kusini na Umoja wa Mataifa zimetangaza kuwa mamia ya maelfu ya raia wa nchi hiyo wanakabiliwa na baa la njaa na wengine milioni moja pia wako katika hatari ya kuathiriwa na janga hilo.