Siku ya Umwagaji Damu nchini Misri
Jumapili ya jana Misri ilikumbwa na hujuma za kigaidi zilizojumuisha milipuko minne ambapo watu karibu 47waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Kufuatia hujuma hizo za kigaidi, Misri imetangaza siku tatu za maombolezo ya umma na rais Abdul Fattah El Sisi ametangaza hali ya hatari na kuamuru jeshi la nchi hiyo lisaidie vikosi vya polisi katika kulinda doria mitaani na maeneo muhimu nchini humo.
Hujuma ya kwanza ilipelekea watu 29 kuuawa na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu dhidi ya Kanisa la Kikhufti (Coptic) katika mji wa Tanta, eneo la Nile Delta. Kanisa lililolengwa linajulikana kama Mar Girgis au Mtakatifu George na lilikuwa limejaa waumini wa Kikristo waliokuwa wakiadhimisha siku ijulikanayo kama Jumapili ya Matawi. Kanisa hilo ni kati ya nembo za kuishi pamoja Waislamu na Wakristo wa Kikhufti nchini Misri. Masaa kadhaa baada ya hujuma hiyo ya Tanta bomu jingine liliripuka nje ya kanisa la Mtakatifu Mark mjini Alexandria ambapo watu 18 wameuawa na wengine karibu 30 kujeruhiwa. Imearifiwa kuwa kiongozi wa Kanisa la Kikhufti Misri alikuwa ndani ya kanisa hilo lakini hakujeruhiwa.
Baada ya Misri kupitia msukosuko wa mwamko wa wananchi wa mwaka 2011, nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na matatizo mengi ya kisiasa, kiuchumi na ukosefu wa usalama. Lakini kuenea makundi ya kigaidi Misri kumeifanya iwe sawa na nchi zingine za eneo ambazo zinasakamwa na jinamizi la ugaidi.
Ingawa Misri imeshuhudia mashambulizi mbali mbali ya kigaidi katika miaka ya hivi karibuni lakini shambulizi la Jumapili na kulengwa kanisa ni kengele ya hatari kubwa kwa nchi hiyo.
Takribani asilimia 10 hadi 15 ya watu wote wa Misri ni Wakristo na wanahesabiwa kama jamii ya waliowachache kidini nchini humo. Hii ni katika hali ambayo kwa miongo kadhaa, Misri ambayo ni makao makuu ya Chuo Kikuu cha Al Azhar ambacho kinahesabiwa kuwa kituo cha masomo ya kidini na kiutamaduni katika nchi za Kiarabu imekuwa ikijinadi kuwa nembo ya kuishi kwa masilikizano wafuasi wa dini mbali mbali wenye mitazamo tafauti ya kisiasa. Serikali pia imekuwa ikisisitiza kuhusu kuishi kwa amani wafuasi wa dini zote nchini humo.
Hata hivyo hujuma ya kigaidi dhidi ya Wakristo Wamisri zimejiri mara kadhaa moja nchini humo na hata kumewahi kutoka hujuma nje ya nchi hiyo. Februari mwaka 2015 kulienezwa kanda ya video ya Wakristo wa Kikhufti wa Msri wakiwa wameuawa kinyama mikononi mwa magaidi wa ISIS katika nchi jirani ya Libya.
Lakini hujuma ya Jumapili katika makanisa mawili nchini Misri ni kilele cha matukio hayo ya kulengwa Wakristo wa Misri. Viongozi mbali mbali wa kidini Misri, wakiwemo viongozi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar wamelaani vikali hujuma hiyo na kutaka chanzo chake kichunguzwe kwa makini.
Misri imekuwa ikichukua misimamo tafuati katika eneo ambayo inaenda kinyume na mitazamo ya Saudi Arabia. Aidha mahakama za Misri hivi karibuni zilibatilisha mapatano ya kuikabidhi Saudia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir katika Bahari ya Sham na hivyo kuzidisha msuguano wa Cairo na Riyadh. Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa hujuma za kigaidi dhidi ya makanisa zinaweza kuwa kwa maslahi ya utawala wa Saudia.
Lakini hakuna shaka kuwa, lengo kuu la hujuma hizo ni kuibua mgawanyiko wa kikaumu na kidini nchini Misri. Iwapo hitilaifu za kidini na kikaumu nchini humo zitashika kasi, basi nchi hiyo itakumbwa na fujo na msukosuko mkubwa. Hali hii itapeleka badhi ya madola makubwa ya Kiarabu kupata fursa ya kujipenyeza na kuvuruga zaidi usalama wa Misri.
Ingawa hujuma hizo zimejiri katika siku kuu ya Wakristo wa Kikhufti na hivyo kuibua hofu na wahka miongoni mwao na kulaaniwa na Waislamu wa nchi hiyo na maeneo mengine duniani, vitendo kama hivyo vya kigaidi kwa hakika ni kinyume cha mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Kwa hakika njama kama hizo za kigaidi zenye kulenga kuleta mifarakano ya kidini zitafeli kwa watu na serikali kuwa angalifu na kutotumbukia kaitka mtego uliowekwa na maadui.