Wahajiri elfu tatu waokolewa katika pwani ya Libya
Maelfu ya wahajiri wamenusurika kufa maji baada ya boti zao kuzama katika bahari ya Mediterania, wakiwa katika juhudi za kuelekea barani Ulaya.
Gadi ya Pwani ya Italia imesema watu elfu 3 waliokolewa jana katika operesheni 35 za kuwanusuru wahamiaji hao, ambao walizama kutokana na boti zao kushindwa kuhimili mawimbi mazito ya bahari.
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka pamoja na asasi zingine zisizo za kiserikali zilizohusika kwenye shughuli za uokoaji zimesema kuwa, wahajiri 2,074 waliokolewa baada ya boti zao 16 za mipira kuzama katika bahari ya Mediterania nyakati za asubuhi huku wengine zaidi ya 1000 wakiokolewa nyakati za usiku.

Timu za waokoaji zimesema aghalabu ya wahajiri hao ni raia wa nchi za eneo la chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika, haswa wanaotoka katika familia masikini.
Haya yanajrii chini ya masaa 48 baada ya wahamiaji wengine 100 kutoweka baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika maji ya pwani mwa Libya wakiwa mbioni kuelekea Ulaya.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu pekee wahajiri zaidi ya 600 wamezama na kufa maji katika bahari ya Mediterania, wakiwa katika safari hatari za kujaribu kuelekea barani Ulaya.