Unicef yafikia maeneo yanakojiri mapigano huko Sudan
Serikali ya Sudan imeruhusu kuingia wataalamu wa Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) katika maeneo yanayojiri mapigano.
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa serikali ya Sudan imetoa kibali na kuwaruhusu wataalamu wa Unicef kuingia katika baadhi ya maeneo kunakojiri mapigano ili kutoa huduma mbalimbali kama kuwalinda raia, kutoa elimu, huduma za afya, lishe bora, maji safi na salama. Serikali ya Sudan miaka mitano iliyopita ilikataa kuwapatia kibali cha kuingia katika maeneo hayo wataalamu wa kimataifa wa Unicef.
Jimbo la Darfur huko magharibi mwa Sudan mwaka 2003 liliathiriwa na mzozo wa ndani na mwaka 2011 na kufuatiwa na mizozo minngine katika majimbo ya Darfur Kusini na Blue Nile. Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa hadi kufikia sasa karibu watu 300,000 wameuawa katika jimbo la Darfur na wengine zaidi ya milioni mbili na laki tano kuwa wakimbizi kufuatia kujiri mapigano katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko huko Sudan.