Apr 23, 2017 14:03 UTC
  • Askari 8 wa Somalia wauawa katika shambulizi la bomu, Puntland

Wanajeshi wanane wameuawa katika mlipuko wa bomu uliotokea katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia.

Duru za habari zinaarifu kuwa, kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa al-Qaeda kupitia msemaji wake Sheikh Abdi Zsis Abu Musab, limekiri kuhusika na shambulizi hilo lililolenga msafara wa magari ya jeshi katika mji wa Galgala, yapata kilomita 40 kusini mwa mji wa Bossaso, katika eneo la Puntland.

Habari zaidi zinasema kuwa, askari watatu wa Puntland wamepata majeraha mabaya katika hujuma hiyo ya kigaidi inayoonekana kuwa ni ya ulipizaji kisasi.

Ramani ya eneo la Puntland

Ijumaa iliyopita, Jeshi la Kenya liliwaua wanamgambo 52 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab katika shambulio lililofanyika kwenye kambi ya kundi hilo huko Badhaadhe, eneo la Juba ya Chini, kusini mwa Somalia.

Kadhalika mapema mwezi huu, Mahakama ya Kijeshi ya Puntland ilitekeleza adhabu ya kifo kwa watu watano wanaoaminika kuwa wanamgambo wenye misimamo ya kufurutu mpaka waliohusika na mauaji ya maafisa watatu waandamizi wa serikali ya eneo hilo. 

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema kuwa, harakati za kundi la kigaidi la al-Shabaab sasa zimepamba moto katika eneo la Puntland baada ya kutimuliwa kwenye ngome zao kusini mwa Somalia na vikosi vya AMISOM vikishirikiana na jeshi la nchi hiyo. 

Tags