UNICEF: Watoto elfu 30 wanahitaji chanjo ya haraka nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28252-unicef_watoto_elfu_30_wanahitaji_chanjo_ya_haraka_nchini_somalia
Mjumbe wa Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) nchini Somalia amesisitizia udharura wa kupatiwa chanjo maelfu ya watoto kusini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 26, 2017 02:32 UTC
  • UNICEF: Watoto elfu 30 wanahitaji chanjo ya haraka nchini Somalia

Mjumbe wa Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) nchini Somalia amesisitizia udharura wa kupatiwa chanjo maelfu ya watoto kusini mwa nchi hiyo.

Steven Lauwerier, amesema kuwa, jumla ya watoto elfu 30 katika mji wa Baidoa, kusini mwa Somalia, bado hawajapata chanjo kwani akthari yao wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na ukame au kwa sababu ya kuishi katika maeneo ya mbali ambayo wahudumu wa mashirika ya afya nchini humo wanashindwa kuyafikia kutokana na mapigano.

Mazingira mabaya ya watoto nchini Somalia

Mwakilishi wa shirika hilo nchini Somalia kadhalika ameelezea kuanza kampeni muhimu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Somalia, Shirika la Afya Duniani (WHO) na asasi kadhaa za kujitegemea iliyoanza jana Jumanne. Kwa mujibu wa afisa huyo wa UNICEF, kampeni hiyo itakuwa ya kugawa chanjo na vitamini D kwa ajili ya kuongeza usalama wa watoto. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, karibu watoto 5700 wameambukizwa ugonjwa wa surua nchini Somalia kiwango ambacho ni cha juu cha maambukizi ya maradhi hayo ikilinganishwa na kila mwaka.

Steven Lauwerier, Mjumbe wa Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) nchini Somalia 

Ijumaa iliyopita taasisi ya kimataifa ya 'Save the Children' ilieleza wasi wasi mkubwa ilionao kutokana na lishe duni inayowakabili watoto wa Somalia na kuonya kuwa, ikiwa hakutachukuliwa hatua za haraka kwa ajili ya kuwadhaminia watoto hao chakula, basi watapoteza maisha hivi karibuni.