Misri yamuhukumu kifo kiongozi wa Ikhwanul Muslimin
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28474-misri_yamuhukumu_kifo_kiongozi_wa_ikhwanul_muslimin
Mahakama moja nchini Misri imemhukumu kifo kiongozi wa harakati ya Kiislamu iliyopigwa marufuku nchini humo ya Ikhwanul Muslimin.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Apr 30, 2017 23:37 UTC
  • Misri yamuhukumu kifo kiongozi wa Ikhwanul Muslimin

Mahakama moja nchini Misri imemhukumu kifo kiongozi wa harakati ya Kiislamu iliyopigwa marufuku nchini humo ya Ikhwanul Muslimin.

Televisheni ya Press TV imeripoti kuwa, Mahakama ya Jinai ya Cairo hapo jana ilimhukumu kifo Wagdi Ghoneim, kiongozi wa Ikhwanul Muslimin mwenye umri wa miaka 66, bila ya yeye kuwepo mahakamani, kwa tuhuma za kuunda eti genge la kigaidi na kuchochea ghasia dhidi ya maafisa usalama wa nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Aprili 2, mahakama hiyo ilitoa hukumu hiyo ya kifo dhidi ya mwanazuoni huyo ambaye anaishi Uturuki, lakini hukumu hiyo ilikuwa ikisubiri kuidhinishwa na Mufti Mkuu wa Misri, Shawki Allam, ambaye ametwikwa jukumu la kutoa kibali cha hukumu zote za vifo nchini humo.

Wanachama wa Ikhwan wakiwa kizimbani mwaka jana

Agosti mwaka jana, mahakama ya kijeshi ya Misri ilitoa hukumu ya vifungo vya kuanzia miaka miwili hadi maisha jela kwa watu 418 ambao ni wanachama na wafuasi wa harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin.

Tangu mwezi Julai 2013 baada ya jeshi likiongozwa na Abdul Fattah al-Sisi kumwondoa madarakani Muhammad Morsi, rais aliyechaguliwa kidemokrasia, utawala wa Misri umekuwa ukitumia mkono wa chuma kuikandamiza vikali harakati ya Ikhwan.

Kwa mujibu wa taasisi za kutetea haki za binadamu, tangu wakati huo hadi hivi sasa, hatua kandamizi za serikali ya el Sisi zimesababisha watu zaidi ya 1,400 kuuawa, 22,000 kufungwa jela na mamia ya wengine kuhukumiwa kifo kwa makundi.