Wananchi waandamana Tunisia kupinga msahama kwa mafisadi
Maelfu ya wananchi wa Tunisia wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo Tunis kupinga muswada ambao ukipasishwa na kuwa sheria, maafisa wa serikali wanaopatikana na hatia ya ufisadi watafutiwa makosa mkabala wa kurejesha mali walizopora kwa dola.
Waandamanaji hao wamesema maafisa wa serikali wanaopatikana na hatia ya rushwa wekiwemo waliohudumu katika serikali iliyopita, sharti wawajibishwe na kufungwa jela.
Asasi zisizo za serikali zaidi ya 50 zimeandaa maandamano hayo chini ya kaulimbiu "Hatusamehi, Ufisadi Hautapita". Hamma Hammami, Kiongozi wa chama cha Popular Front amesema: "Hakuna mapatano na mafisadi bila kufichuliwa ukweli na mafisadi hao kupandishwa kizimbani na kuhukumiwa vifungo jela."
Maandamano hayo ya jana Jumamosi yanafananishwa na yale yaliyofanyika nchini humo miaka sita iliyopita, ambayo yalimuondoa madarakani dikteta wa muda mrefu wa nchi hiyo, Zainul Abiddin Bin Ali.
Siku chache ziliopita, Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia aliamuru jeshi la nchi hiyo kulinda vituo vya kuchimba gesi na mafua baada ya waandamanaji kujaribu kuvuruga uzalishaji katika vituo hivyo vilivyoko kusini mwa nchi.
Tunisia inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi na ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana wa kusini mwa nchi hiyo ambao wanahisi kutengwa na serikali.