UNICEF yatoa indhari ya watoto kubaki bila ya walezi Magharibi mwa Afrika
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kushughulikia Watoto UNICEF umetangaza kuwa kati ya kila watoto watano, mmoja amepoteza wazazi wake wote wawili kutokana na ugonjwa wa Ukimwi magharibi mwa Afrika.
UNICEF imeongeza kuwa, mbali na majonzi ya kuondokewa na wazazi, watoto hao wanabeba pia mzigo wa kuvumilia ghamu na machungu ya kutengwa na jamaa wengine wa familia pamoja na majirani.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kushughulikia Watoto, kwa kutoa mfano, katika eneo la kaskazini mwa Togo ambayo ni moja ya nchi ndogo zaidi barani Afrika watoto zaidi ya 60 wanaishi peke yao katika hali ya ufukara huku msaada pekee wanaopata ukiwa ni wa mashirika ya misaada ya kibinadamu.
Ripoti ya UNICEF aidha imefafanua kuwa nchini Togo, watoto ambao wanaondokewa na wazazi wao kutokana na ukimwi wanahifadhiwa kwenye kituo pekee cha kushughulikia watoto hao kilichoko nchini humo.
Ugonjwa wa ukimwi unaosababishwa na virusi vya HIV ni ugonjwa wa kuambukiza ambao kidogokidogo umegeuka kuwa moja ya vizuizi vikubwa vya kupatikana ustawi wa uchumi na kuwa na serikali endelevu katika bara la Afrika.../