May 19, 2017 07:30 UTC
  • Makumi wauawa katika mapigano ya makundi hasimu Libya

Makumi ya watu wameuawa baada ya vikosi tiifu kwa makundi hasimu ya kisiasa nchini Libya kukabiliana huko kusini mwa nchi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kwa akali watu 60 wameuawa katika mapigano hayo yaliyofanyika jana Alkhamisi baada ya kikosi cha jeshi kutoka mji wa magharibi mwa Misrata kuvamia kituo cha jeshi kilichoko katika mji wa Brak Al-Shati.

Meya wa Brak Al-Shati, Ibrahim Zemmi, amesema askari wa Kikosi cha 12 pekee waliouawa katika mapigano hayo ni zaidi ya 70, huku wengine 18 wakijeruhiwa. Naye Mohamed Al-Afirs, Msemaji wa Kikosi cha 12 amesema waliouawa ni watu zaidi ya 86 wakiwemo wanajeshi na raia. 

Duru za hospitali katika mji wa Brak Al-Shati zinasema yumkini idadi hiyo ikaongezeka kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata baadhi ya askari, huku taharuki ya kuendelea mapigano hayo ikitanda kusini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. 

Mapigano hayo yanajiri katika hali ambayo, mapema mwezi huu, Khalifa Haftar, Mkuu wa Jeshi la Libya mashariki mwa nchi hiyo na Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya walikutana mjini Abu Dhabi, Imarati na kufikia makubaliano kuhusu utatuzi wa hitilafu za pande hizo mbili. Viongozi hao wawili walikubaliana pia kuunda jeshi moja na kusimamia kwa pamoja uchaguzi wa Rais na Bunge katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Mbali na mapigano kati ya vikosi hasimu, genge la Daesh pia limevuruga usalama wa Libya

Ieleweke kuwa, Libya kwa muda mrefu imekuwa na serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk na nyingine ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. 

Tangu mwaka 2011 na baada ya kuangushwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gadafi, Libya imegeuka uwanja wa mapigano, machafuko na kuvurugika uthabiti wa kisiasa.

Tags