Kuendelea kutolewa hukumu za ajabu na idara ya mahakama ya Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29410-kuendelea_kutolewa_hukumu_za_ajabu_na_idara_ya_mahakama_ya_misri
Katika hali ambayo idara ya mahakama ya Misri imemtoa hatiani dikteta Hosni Mubarak, rais wa zamani wa nchi hiyo kwa makosa yote aliyofanya yakiwemo hata mashtaka ya kuua watu wakati wa mapinduzi ya wananchi mwaka 2011, Mahakama Kuu ya Misri imemuweka kwenye orodha ya magaidi Muhammad Morsi, rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa na wananchi na baadaye kupinduliwa na jeshi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2017 02:16 UTC
  • Mohammad Morsi, rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kidemokrasia. Amefungwa jela baada ya kupinduliwa na jeshi.
    Mohammad Morsi, rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kidemokrasia. Amefungwa jela baada ya kupinduliwa na jeshi.

Katika hali ambayo idara ya mahakama ya Misri imemtoa hatiani dikteta Hosni Mubarak, rais wa zamani wa nchi hiyo kwa makosa yote aliyofanya yakiwemo hata mashtaka ya kuua watu wakati wa mapinduzi ya wananchi mwaka 2011, Mahakama Kuu ya Misri imemuweka kwenye orodha ya magaidi Muhammad Morsi, rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa na wananchi na baadaye kupinduliwa na jeshi.

Siku ya Jumamosi ya tarehe 20 Mei, Mahakama Kuu ya Misri iliwaingiza Muhammad Morsi, rais wa zamani wa nchi hiyo pamoja na Muhammad Badei, mkuu wa Ikhwanul Muslimin na wanachama wengine 24 wa kundi hilo, katika orodha ya magaidi.

Tunapoangalia matukio ya hivi karibuni ya Misri tutaona kuwa, mfumo wa mahakama wa nchi hiyo, daima unafuata amri kutoka kwa serikali iliyoko madarakani. Namna idara ya mahakama ya Misri ilivyofuatilia kesi ya dikteta Hosni Mubarak na wanawe, inatofautiana kikamilifu na ufuatiliaji wake wa kesi za Muhammad Morsi na viongozi wengine wa Ikhwanul Muslimin.

Dikteta Hosni Mubarak akiwa mahakamani na wanawe wawili Ala'a na Gamal. Wana nyuso za bashasha na hawaonekani kuwa na wasiwasi wowote 

 

Mwaka 2011 idara ya mahakama ya Misri ilianza kufuatilia kesi ya Hosni Mubarak na baadhi ya wajumbe wa utawala wake wa kiimla katika hali ambayo, haikuwa ikiwaangalia kuwa ni watuhumiwa, bali kama marafiki. Husni Mubarak na wanawe wawili Ala'a na Gamal walikuwa wanakabiliwa na tuhuma za kuhusika na mauaji ya waandamanaji katika kipindi chote cha kampeni ya mapinduzi ya Januari 25 yaliyoung'oa madarakani utawala wake wa kidikteta. Tuhuma nyingine zilizoukabili utawala kibaraka wa Hosni Mubarak ilikuwa ni ubadhirifu wa mali za umma. Hata hivyo, hadi wakati huo, wafuasi wa Hosni Mubarak walikuwa na nafasi muhimu katika Baraza Kuu la kijeshi la Misri. 

Hivyo kama ilivyotarajiwa, hukumu zilizotolewa na mahakama ya Misri dhidi ya Mubarak na wanawe zilikuwa za ajabu sana na hazikuwa na chembe ya uadilifu. Kwanza mahakama hiyo iliwatoa hatiani watoto wa Hosni Mubarak, Ala'a na Gamal, halafu ikadai kuwa Hosni Mubarak ana kesi ya kujibu kuhusu mauaji ya waandamanaji katika kampeni ya mapinduzi ya Januari 25. Hosni Mubarak akakata rufaa mara moja kupinga huku hiyo dhidi yake. Wakati huo wanachama wa Ikhwanul Muslimin walikuwa wamepata ushindi katika uchaguzi wa bunge la Misri na Muhammad Morsi akawa amekaribia kushinda uchaguzi wa rais.

Awamu ya pili ya kesi ya dikteta Hosni Mubarak ilianza baada ya kupinduliwa serikali ya Muhammad Morsi na ya kundi la Ikhwanul Muslim. Kupinduliwa serikali hiyo kuliathiri moja kwa moja usikilizaji wa kesi ya Hosni Mubarak, kwani wapinzani wake wakuu walikuwa hawako tena madarakani. Hivyo mwaka 2014, mahakama ya Misri ilitoa hukumu ya ajabu dhidi ya Hosni Mubarak, ya kifungo cha miaka mitatu tu jela kwa tuhuma nzito ya kufilisi mali za umma na kujijengea majumba ya kifakhari. Muda wa kifungo hicho umemalizika mwezi huu wa Mei 2017 na hivi sasa dikteta huyo ameachiliwa huru. Ikumbukwe kuwa wakati wa kutolewa hukumu hiyo yaani mwezi Mei 2014, serikali ya Misri ilikuwa mikononi mwa Adel Mansour, mfuasi wa karibu wa Hosni Mubarak.

Wananchi wa Misri wakikabiliwa na ukandamizaji wa polisi wakati wa maandamano

Sasa tuje katika upande wa kesi za Muhammad Morsi na viongozi wengine wa Ikhwanul Muslimin. Usikilizaji wa kesi hizo umeathiriwa moja kwa moja na msimamo wa serikali iliyoko madarakani. Muhammad Morsi na viongozi wengine wa Ikhwanul Muslimin wametuhumiwa kuchochea machafuko na kufanya ujasusi, huku serikali ya Jenerali Abdel Fattah el Sisi ikidai kuwa Ikhwanul Muslimin ni kundi la kigaidi. Hukumu zilizotolewa na mahakama ya Misri dhidi ya Muhammad Morsi na viongozi wengine wa Ikhwanul Muslimin, zimefuata msimamo huo huo wa serikali ya Cairo. Cha ajabu zaidi ni kwamba, Muhammad Morsi na viongozi wengine wa Ikhwanul Muslimin walishahukumiwa vifungo vya miaka mingi jela ikiwa ni pamoja na kifungo cha miaka 20 dhidi ya Morsi kwa tuhuma za kuchochea tu machafuko. Lakini Hosni Mubarak na wanawe waliokuwa na tuhuma za kufanya mauaji, wamesamehewa.  Hivi sasa pia idara ya mahakama ya Misri imefuata siasa za serikali za kuwaingiza Muhammad Morsi na baadhi ya viongozi wa Ikhwanul Muslimin katika orodha ya magaidi.

Hukumu za namna hiyo zinathibitisha wazi kuwa, mfumo wa mahakama wa Misri hauna uadilifu hata chembe, bali unafuata tu matakwa na maslahi ya serikali iliyoko madarakani.