May 27, 2017 10:51 UTC
  • Shambulio la kigaidi nchini Misri

Watu wasiopungua 28 waliuawa nchini Misri na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la jana Ijumaa dhidi ya mabasi mawili yaliyokuwa yamewabeba Wakristo wa Kibti kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Cairo.

Gavana wa mkoa wa Minya, Essam el-Bedawi amesema kuwa, shambulio hilo dhidi ya mabasi hayo lilifanywa na watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha. Akthari ya wahanga wa shambulio hilo la jana huko Minya Misri ni watoto wadogo. Baada ya shambulio hilo la kigaidi, Jeshi la Anga la Misri limefanya mashambulio dhidi ya kambi za mafunzo ya magaidi katika mji wa Derna ambao kijiografia unapatikana kaskazini mashariki mwa Libya.

Kwa hakika hii si mara ya kwanza kwa Misri kuandamwa na mashambulio ya kigaidi katika miezi ya hivi karibuni. Hivi karibuni makanisa mawili ya Wakristo wa Kibti yalishambuliwa wakati Wakristo hao walipokuwa wakiadhimisha sikukuu yao, ambapo makumi ya ya watu waliuawa na kujeruhiwa. Hata kama Misri baada ya vuguvugu la mapinduzi ya wananchi la mwaka 2011 kwa kiwango fulani imeweza kurejesha amani na utulivu, lakini kubadilika mazingira ya kisiasa katika nchi nyingine za eneo kwa upande mmoja, na kushadidi hitilafu za kisiasa ndani ya nchi hiyo kwa upande wa pili, ni mambo ambayo kwa muda sasa yameifanya Misri iendelee kushuhudia ukosefu wa amani na utulivu sambamba na kuongezeka mivutano ya kisiasa, kikaumu na kimadhehebu.

Wanachama wa kundi la wauaji la Daesh

Katika upande mwingine Misri inakabiliwa na tatizo la uchumi. Kuongezeka umasikini, ukosefu wa ajira sanjari na kushadidi ugumu wa maisha, ni mambo ambayo kwa hakika yameyafanya maisha ya Wamisri yazidi kuwa magumu kila siku iendayo kwa Mungu. Majimui ya hali hii yamepelekea Misri iwe katika faharasa ya nchi zinazolengwa na makundi ya kigaidi likiwemo kundi la wauaji la Daesh. Hivi sasa kupanuka wigo wa harakati za makundi ya kigaidi nchini Misri kama ilivyo kwa baadhi ya nchi za eneo la kaskazini mwa Afrika limekuwa ni tatizo na tishio kubwa. Inavyoonekana ni kuwa, kuongezeka vitendo vya kigaidi nchini Misri kunapaswa kutazamwa katika kona mbili za ndani na nje.

Katika upande wa ndani ni kuwa, kujihusisha na hitilafu za kidini na kimadhehebu ni moja ya mambo yenye taathira hasi katika kuzusha hitilafu na kuzorotesha hali ya mambo. Wakristo wanaunda takriban asilimia 10 hadi 15 ya wakazi wa Misri na wanahesabiwa kuwa wafuasi wa dini za walio wachache. Kwa miaka nenda rudi, Wakristo wamekuwa wakiishi salama salimini na wafuasi wa dini nyingine. Pamoja na hayo, katika miaka ya hivi karibuni sambamba na kuongezeka uwepo wa makundi ya kigaidi katika eneo hili na kuchukua wigo mpana jinai zao, kukuza hitilafu za kidini na kulitumia jambo hilo kama wenzo wa kufikia malengo, ni mambo ambayo yamekuwa yakitumiwa na makundi hayo ya kigaidi. 

Rais Abdul-Fattah al-Sisi wa Misri

Katika upande mwingine mizozo ya kisiasa baina ya vyama vya nchi hiyo na misimamo ya ndani nayo imepelekea kujitokeza ufa katika jamii ya Wamisiri jambo ambalo limeyaandalia uwanja na fursa makundi ya kigaidi ya kulitumia suala hilo kwa ajili ya kufikia malengo yao. Katika upande wa nje ni kuwa, mazingira ya eneo hili na hali isiyo na amani na utulivu ya nchi zinazopakana na Misri, kutokuweko serikali yenye nguvu katika nchi kama Libya na vile vile kuweko vyanzo vya utajiri wa maliasili ni mambo ambayo nayo yameandaa uwanja wa kushuhudiwa ongezeko la harakati za makundi ya kigaidi nchini humo. Aidha katika upande mwingine, baadhi ya makundi hayo yamekuwa yakipata uungaji mkono wa siri wa baadhi ya nchi za eneo hili na ndio maana yanaonekana wazi kuwa lengo lao ni kutekeleza siasa za nchi hizo jambo ambalo nalo limechochea moto wa mizozo nchini Misri.

Viongozi wa Misri kwa mara nyingine tena sambamba na kulaani hujuma hiyo ya kigaidi na mfano wake, wamesisitizia udharura wa kupambana na ugaidi. Pamoja na kuwa, siasa hizi na vitendo vya ugaidi vitashindwa na kugonga mwamba, lakini kuleta anga tulivu ndani ya Misri na vile vile kurejesha amani na utulivu wa kieneo, ni hatua ambazo bila ya shaka zitafunga milango ya harakati za makundi ya kigaidi.

Tags