Jun 05, 2017 14:09 UTC
  • Kituo cha polisi chashambuliwa Somalia, 23 wauawa na kujeruhiwa

Watu watatu wameuawa na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa katika shambulizi la guruneti dhidi ya kituo cha polisi nchini Somalia mapema leo Jumatatu.

Idhaa ya serikali ya nchi hiyo imeripoti kuwa, hujuma hiyo inayooaminika kuwa ya kigaidi imetokea katika mji wa bandari wa Kismayu, yapata kilomita 500 kusini mwa mji mkuu, Mogadishu.

Habari zaidi zinasema kuwa, maafisa usalama na wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM walifika mara moja katika kituo hicho baada ya kuripotiwa mripuko huo na tayari wameanzisha uchunguzi kubaini wahusika.

Wanachama wa genge la ukufurishaji la al-Shabaab

Duru za kiusalama katika eneo la Jubaland zinasema maafisa usalama ni miongoni mwa waliojeruhiwa kwenye mripuko huo.

Hadi tunaenda mitamboni, hakuna genge lolote lililokuwa limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ingawaje inatazamiwa kuwa shambulizi hilo limetekelezwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab. 

Hivi karibuni Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo alitoa msamaha wa siku 60 kwa wanamgambo wa al-Shabaab ambao wataweka silaha chini na kujisalimisha kwa serikali.  

Kufuatia msahama huo, wiki iliyopita Bishar Mumin Afrah, kamanda mmoja mwandamizi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab alijisalimisha kwa jeshi la taifa la Somalia, katika mji wa Buloburte ulio eneo la Hiran, yapata kilomita 200 kaskazini mwa Mogadishu. 

Tags