Jul 01, 2017 06:33 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika mapigano ya ndani CAR

Mapigano yanayojiri nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yamesababisha vifo vya watu wawili na kujeruhiwa wengine wanne.

Djerassem Mbaiorem mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) huko Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, watu wawili wameuawa, wanne kujeruhiwa na wengine elfu tatu na mia tano kukosa makazi yao katika eneo la Zemio kusini mwa nchi hiyo kufuatia mapigano yaliyoanza nchini humo Jumanne iliyopita. 

Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliokosa makazi baada ya nyumba zao kuchomwa moto  

 Meya wa mji wa Zemio unaopatikana karibu na mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa, watu wasiojulikana wamefanya uporaji katika maduka na nyumba katika mji huo na kisha kuzichoma moto nyumba hizo.

Tarehe 14 mwezi Aprili uliopita watu waliokuwa na silaha walishambulia kambi ya kikosi cha askari wa kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mji wa Zimiu. Kabla ya hapo pia wanajeshi wawili wa kofia bluu wa Umoja wa Mataifa waliuawa katika shambulizi lililofanywa mwezi Januari mwaka huu dhidi ya msafara wao kati ya mji wa Zemio na Obo mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Askari jeshi wa kudumisha amani wakipiga doria katika mji wa Obo, Jamhuri ya Afrika ya Kati   

 

Tags