Aug 06, 2017 16:23 UTC
  • Mapigano makubwa ya kikabila yatokea katika mkoa wa Tanganyika DRC

Msemaji wa Jumuiya ya Kiraia ya mkoa wa Tanganyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza kuwa, kumetokea mapigano makubwa ya kikabila katika mkoa huo ambayo yamesababisha umwagaji damu mkubwa.

Kwa mujibu wa maafisa wa mkoa wa Tanganyika, mapigano hayo ya kikabila yameripotiwa kuibuka kati ya makabila mawili ya Luba na jamii ya mbilikimo.

Duru za usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimetangaza kuwa, zaidi ya watu 50 wameuawa katika mapigano hayo ya kutisha huku wengine 30 wakijeruhiwa.

Hadi sasa chanzo cha mapigano hayo bado hakijajulikana, ingawa duru za habari zinasema kuwa, makabila hayo yamekuwa na uhasama wa muda mrefu na mara kwa mara kumekuwa kukizuka mapigano.

Makaburi mengi ya umati yamegunduliwa katika mji wa Kasai

Inaelezwa, makumi ya watu wameuawa hadi sasa tangu kuanza tena mapigano katika mkoa wa Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Julai mwaka jana.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu yameendelea kutahadharisha kuhusu hali kuzidi kuwa mbaya katika mikoa miwili ya Tanganyika na Kasai.

Hivi karibuni Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lilitangaza habari ya kuweko wakimbizi milioni mbili katika mikoa miwili ya Tanganyika, mashariki mwa nchi na Kasaï, katikati mwa taifa hilo.

Tags