Aug 23, 2017 03:47 UTC
  • UNICEF: Mashambulio ya Boko Haram kwa kutumia watoto wanaojiripua yameongezeka mara nne

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kuhudumia watoto UNICEF umetangaza kuwa idadi ya watoto wanaotumiwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram nchini Nigeria kufanya mashambulio ya kujitoa mhanga imeongezeka mara nne mwaka huu kulinganisha na mwaka uliopita wa 2016.

Taarifa iliyotolewa na UNICEF imeeleza kuwa tangu mwezi Januari hadi sasa Boko Haram limewatumia watoto 83 kufanya mashambulio ya kigaidi kwa kujifunga mada za miripuko, 55 wakiwa ni wasichana wenye takribani umri chini ya miaka 15 na wavulana 27. Mmoja wa washambuliaji hao ni kitoto kichanga kilichofungashwa na msichana. Kwa mujibu wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kuhudumia watoto, Boko Haram lilitumia watoto 19 katika mashambulio ya kigaidi liliyofanya mwaka uliopita.

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram

Taarifa ya UNICEF imeeleza kuwa taasisi hiyo ina wasiwasi mkubwa kutokana na ongezeko kubwa la utumiaji kikatili na kimahesabu watoto wadogo hususan wasichana kama 'mabomu watu' huko kaskazini mashariki mwa Nigeria, na kusisitiza kuwa kuwatumia watoto namna hiyo ni ukatili wa kupindukia.

 Kwa mujibu wa vyombo vya habari, wimbi la mashambulio ya kujitoa mhanga yanayofanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limeongezeka kaskazini mashariki mwa Nigeria katika kipindi cha wiki chache zilizopita ambapo tangu Juni Mosi mwaka huu hadi sasa watu wasiopungua 170 wameuawa katika mashambulio hayo…/

 

Tags