Sep 11, 2017 03:19 UTC
  • Washukiwa sita wa ugaidi watiwa mbaroni Algeria

Maafisa wa kulinda usalama nchini Algeria wamewatia mbaroni watu sita wanaoshukiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi.

Wizara ya Ulinzi ya Algeria imetangaza kuwa, vikosi vya kulinda usalama vya nchi hiyo vinaendelea na operesheni ya kupambana na ugaidi na kuwasaka washukiwa wa shambulio la kigaidi lililotokea katika kituo cha usalama cha mji wa Tiaret ulioko umbali wa kilomita 300 magharibi mwa mji mkuu, Algiers.

Wizara ya Ulinzi ya Algeria imeongeza kuwa, watuhumiwa wanne kati ya hao walitiwa mbaroni jana Jumapili na wawili walikamatwa siku ya Ijumaa.

Maafisa wa serikali ya Algeria wakilichunguza eneo ulipotokea mripuko katika mji wa Tiaret

 

Uchunguzi wa maafisa usalama wa Algeria unaonesha kuwa shambulio hilo lilipoangwa na kufanywa na kundi moja la kigaidi lililopata mafunzo nje ya Algeria.

Kabla ya hapo wataalamu wa Algeria walikuwa wametangaza kuwa, mada zilizotumiwa katika shambulio hilo kwenye mji wa Tiaret zinaonesha kuwa magaidi waliofanya shambulizi hilo ni wale waliokuweko Syria na Iraq. Kwa mujibu wa wataalamu hao, hadi hivi sasa mkanda wa mabomu uliotumiwa katika shambulizi hilo haujawahi kutumiwa nchini Algeria na ni aina ya mikanda ya kujiripua kwa mabomu inayotumiwa na magaidi katika nchi za Syria na Iraq.

Tags