Sep 18, 2017 04:01 UTC
  • Mapigano yapamba moto kaskazini magharibi mwa Libya

Mapigano makali yamepamba moto kati ya makundi hasimu katika mji wa Misrata wa kaskazini magharibi mwa Libya. Mtu mmoja ameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Mtandao wa habari wa "Bawwabat Afriqiyyal Ikhbariyya" umemnukuu afisa mmoja wa jeshi la Libya akisema kuwa, mapigano hayo yaliyotokea jana mjini Misrata yamepelekea mtu mmoja kuuawa na wengine saba kujeruhiwa.

Afisa huyo wa kijeshi wa Libya ameongeza kuwa, makundi hayo mawili yameshambuliana kwa kutumia silaha mbalimbali za kivita yakiwemo maroketi.

Mapigano ya ndani yameangamiza kila kitu nchini Libya

 

Watu walioshuhudia wamesema kuwa, baadhi ya makundi yenye silaha nchini Libya yanatumia watunga shabaha stadi kushambulia wapinzani wao. Mji wa Misrata una karibu wakazi elfu tisa. 

Libya ilitumbukiwa kwenye machafuko mwaka 2011 baada ya shirika la kijeshi la nchi za magharibi NATO kuishambulia kikatili nchi hiyo katika kampeni za kumpinduwa Kanali Muammar Gaddafi.

Tangu wakati huo hadi hivi sasa, Libya haijawahi kushuhudia utulivu wa aina yoyote ile kiasi kwamba sasa hivi kuna mabunge mawili tofauti nchini humo, moja linaungwa mkono na jeshi la taifa linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar na bunge jingine linaungwa mkono na serikali wa mpito wa Faez Sarraj inayoungwa mkono na nchi za Magharibi ikiwemo Marekani.

Tags