Sep 29, 2017 02:34 UTC
  • Kugeuka bunge la Uganda uwanja wa kurushiana makonde

Mpango wa kuondolewa ukomo wa umri wa rais kwa ajili ya kumuwezesha Rais Yoweri Museven wa Uganda kugombea tena katika uchaguzi wa rais ujao, umepelekea bunge la nchi hiyo kukumbwa na hali ya mchafukoge.

Vurugu na kutwangana makonde katika bunge la Uganda vimejiri katika hali ambayo wabunge wanaounga mkono na wale wanaopinga mpango huo walikuwa wakijadili kwa siku ya pili pendekezo la kumruhusu Rais Museveni kugombea urais na kuweza kuendelea kusalia madarakani kwa ajili ya muhula mwingine. Kwa mujibu wa katiba ya Uganda, ukomo wa rais ni miaka 75, na kwa msingi huo Rais Museven ambaye hadi sasa ana umri wa miaka 72, hatoruhusiwa kugombea tena katika uchaguzi ujao wa rais. Museveni amekuwa madarakani nchini Uganda tangu mwaka 1986 na hivyo kuwa miongoni mwa viongozi waliosalia zaidi madarakani barani Afrika.

Bunge la Uganda kabla ya kubadilika kuwa uwanja wa masumbwi

Mwaka 2005, rais huyo sambamba na kuifanyia mabadiliko katiba ya Uganda na kuondoa kipengee cha ukomo wa mihula miwili, alijifungulia njia ya kuendelea kusalia madarakani. Katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 na licha ya malalamiko makubwa ya wapinzani waliokituhumu chama tawala NRM kwamba kilifanya uchakachuaji mkubwa katika uchaguzi wa rais, lakini kwa uamuzi uliopitishwa na Mahkama Kuu, kwa mara nyingine Museveni aliapishwa kuwa rais wa Uganda. Kwa muda sasa wakosoaji wa Museveni wamekuwa wakimtuhumu rais huyo kuwa anapanga kuwa rais wa maisha wa Uganda, sambamba na kumuandalia mazingira mtoto wake wa kiume kushika uongozi baada yake.

Rais Yoweri Museven wa Uganda anayekosolewa na wapinzani

Kwa mujibu wa wakosoaji hao, kubadilisha katiba na kuondoshwa kipengee cha ukomo wa mihula miwili ya urais, ilikuwa ni hatua yake ya kwanza katika uwanja huo na sasa katika hatua nyingine, chama tawala kinafanya juhudi za kumuondolea ukomo wa umri na hivyo kumfanya aweze kusalia madarakani zaidi nchini humo. Kadhalika wakosoaji wanakituhumu chama tawala kuwa kinabinya uhuru wa kisiasa na uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda. Katika uwanja huo Francois Lounceny Fall, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la katikati mwa Afrika anaamini kuwa: "Migogoro endelevu ya kisiasa katika baadhi ya nchi za Afrika, kimsingi inasababishwa na mwenendo wa chaguzi ambazo zinahesabiwa kuwa kizuizi kikuu cha njia ya kufikia amani katika nchi hizo." Kubadilisha katiba na kuondolewa kikomo cha umri na mihula kwa ajili ya rais, ni njia mbili kuu zinazotumiwa katika miaka ya hivi karibuni na viongozi wengi wa Afrika kwa ajili ya kuendelea kusalia zaidi madarakani. Suala hilo katika nchi nyingi za bara hilo limekuwa kichocheo kikubwa cha mivutano kati ya watawala na wapinzani na hatimaye kupelekea machafuko na ukosefu wa usalama au wakati mwingine kuishia kuundwa tawala za kidikteta.

Dakta Kizza Besigye mpinzani wa Rais Yoweri Museven wa Uganda akipigwa na polisi

Hata kama katika kujaribu kudumisha demokrasia, vyama vya siasa katika baadhi ya nchi vinaonekana kufanya juhudi katika uwanja huo, hata hivyo vitisho na kamatakamata na uwekaji korokoroni unaofanywa na serikali za vyama tawala dhidi ya wapinzani na kukosekana mshikamano madhubuti baina ya vyama vya upinzani kumevifanya vyama hivyo vishindwe kupata mafanikio kamili katika jitihada za kurasimisha demokrasia katika nchi zao. Kuhusiana na suala hilo, Bi Nkosazana Dlamini-Zuma, Mkuu wa zamani wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, sambamba na kuwaonya viongozi wa nchi za bara hilo, amewataka waimarishe demokrasia na kuheshimu haki za binaadamu huku akisisitiza kuwa, kukosekana hali ya kuaminiana kati ya serikali na wananchi, kunalifanya bara la Afrika likabiliwe na matatizo makubwa. Katika hali ambayo akthari ya nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na hatari ya ongezeko la makundi ya kigaidi na ukosefu wa usalama pamoja na matatizo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, kuongezeka tofauti na machafuko ya ndani, kunaweza kuyafanya maisha ya wakazi wa bara hilo kuwa magumu zaidi.

Tags