Sep 30, 2017 16:26 UTC
  • Watu karibu 11 wauawa katika ufyatuaji risasi Afrika Kusini

Polisi ya Afrika Kusini imeripoti kuwa, watu karibu 11 wameaga dunia katika mlolongo wa vitendo vya kufyatuana risasi vilivyotokea usiku wa kuamkia leo katika mji wa Cape Town wakiwemo watu wanne waliouliwa kwa kupigwa risasi kwenye baa moja.

Msemaji wa Polisi ya Afrika Kusini, Novela Potelwa amesema kuwa maafisa kadhaa wa polisi wamesambazwa katika wilaya ya Philipi huko Cape Town kujaribu kudhibiti hali ya mambo. Mji huo umekuwa ukikumbwa na machafuko ya mara kwa mara na mashambulizi ya silaha kati ya magenge ya wahalifu. Msemaji huyo wa Polisi ya Afrika kusini amesema, jeshi hilo linafanya juhudi za kuwatia mbaroni wahusika wa mauaji hayo. Watu wanne waliuliwa jana jioni kwa kupigwa risasi wakiwa ndani ya baa moja katika kitongoji cha Philipi huku miili ya watu wengine watatu ikikutwa imetelekezwa katika eneo jirani.

Polisi wakiwa katika msako mahali palipojiri ufyatuaji huo huko Cape Town 

Polisi imesema, watu wengine watatu waliuawa katika maeneo tofauti wilayani humo. Chama tawala cha Afrika Kusini ANC kimelaani mauaji hayo kikisema kuwa ni jinai ambayo watendaji wake wanapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Takwimu zilizotolewa mwaka jana zilionyesha kuwa, kwa wastani kila siku kunatokea mauaji ya watu 51 huko Afrika Kusini.  Wiki iliyopita pia watalii wa Kiholanzi waliibiwa vitu vyao walipokuwa ndani ya basi wakielekea hotelini baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Johannesburg kwa ajili ya mapumziko ya wiki tatu.

Tags