Oct 01, 2017 03:56 UTC
  • Serikali ya Niger yawaonya wafanyabiashara wanaoshirikiana na Boko Haram

Viongozi wa Niger wamewaonya vikali wafanyabiashara ambao wanafanya biashara kwa siri na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Shirika la habari la Ufaransa limewanukuu viongozi wa Niger wakitoa onyo hilo jana katika kikao cha makamanda wa jeshi la nchi hiyo na wafanyabiashara wa eneo la Diffa la kusini mwa Niger na kusema kuwa, wanatoa onyo la mwisho kwa watu ambao wanawadhiminia Boko Haram mahitaji yao kwa njia ya siri.

Magaidi wa Boko Haram wanafanya jinai kubwa nchini Niger

 

Viongozi wa Niger wamesisitiza kuwa, kila anayeshirikiana na genge la kigaidi la Boko Haram anapaswa kuacha mara moja kufanya hivyo kwani mtu huyo hana tofauti yoyote na magaidi wa kundi hilo wanaofanya jinai za kutisha dhidi ya raia.

Vile vile wameonya kuwa, kuanzia sasa mtu yeyote anayeshirikiana na Boko Haram kwa njia yoyote ile atahesabiwa kuwa ni sawa na magaidi wa kundi hilo na hatua kali dhidi yake zitachukuliwa kwa kiwango hicho hicho.

Hadi hivi sasa nchi za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon zimeshindwa kuwamaliza magaidi wa Boko Haram na moja ya sababu zinazotolewa ni kwamba baadhi ya wenyeweji wa maeneo waliko Boko Haram wanashirikiana kwa siri na magaidi hao.

Tags