Oct 03, 2017 08:12 UTC
  • Watu 16 wauawa katika mapigano mashariki mwa Kongo DR

Kwa akali wanachama 16 wa kundi la waasi wa Mai-Mai wameuawa katika mapigano na maafisa usalama, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Duru za kijeshi zimeripoti kuwa, mapigano kati ya pande mbili hizo yamekuwa yakiendelea katika kitongoji cha Kipese mjini Lubero, katika mkoa wa Kivu Kaskazini tangu Ijumaa iliyopita.

Msemaji wa Jeshi la DRC, Jules Tshikudi amesema wapiganaji wanne wa kundi hilo waliuawa Ijumaa, saba wakaangamizwa katika makabiliano ya Jumapili huku miili ya wengine watano ikipatikana jana Jumatatu.

Hata hivyo amesisitiza kuwa, kwa sasa hali ya mambo imedhibitiwa baada ya kuuawa wanachama hao wa genge la waasi wa Mai Mai.

Waasi wa Mai-Mai

Itakumbukwa kuwa, Agosti mwaka jana, makundi yanayobeba silaha kwa jina la Muungano kwa Ajili ya Kongo Iliyo Huru  na waasi wa Mai-Mai walikubali kusitisha mashambulizi yao katika eneo la Masisi mkoani Kivu Kaskazini.

Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanashuhudia machafuko na mapigano kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, mgogoro usioisha wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unachochewa na madola ya kigeni yanayoangalia kwa macho ya tamaa utajiri mkubwa wa maliasi wa nchi hiyo hususan madini.

 

Tags