Jeshi la Misri laangamiza wanachama 24 wa Daesh eneo la Sinai
Jeshi la Misri limetangaza habari ya kuwaua wanachama 24 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika Peninsula ya Sinai, kaskazini mwa nchi.
Taarifa ya jeshi hilo inasema kuwa, magaidi hao wakufurishaji walishambuliwa na kuangamizwa baada ya kujaribu kuvamia kituo cha kijeshi kusini mwa mji wa Sheikh Zuweid, kwa mabomu ya kutegwa garini na maguruneti.
Habari zaidi zinasema kuwa, wanajeshi 6 wa Misri wameuawa huku wengine 20 wakijeruhiwa katika makabiliano hayo ya jana Jumapili yanayoonekana kuwa ya ulipizaji kisasi.
Hii ni katika hali ambayo, Ijumaa iliyopita, jeshi la Misri lilitoa taarifa na kusema kuwa, "magaidi waliokuwa na silaha wameshambulia kituo cha jeshi katika mji wa Arish kwa kutumia bunduki na mabomu ya mkononi na kuua wanajeshi sita."
Eneo hilo la kaskazini mwa Misri limekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha kwa miaka kadhaa sasa. Kundi hatari zaidi ni lile linalojiita Ansar Bait al-Muqaddas ambalo limetangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS).
Eneo hilo halijawahi kuwa na utulivu tangu magenge ya kigaidi yaanzishe harakati zao mwaka 2013, baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani kwa nguvu Mohamed Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.