Ethiopia kuendelea kushirikiana na Somalia katika vita dhidi ya al-Shabaab
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Somalia katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab.
Desalegn aliyasema hayo katika mazungumzo na Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed ambaye yuko mjini Addis Ababa na kuongeza kuwa, nchi mbili hizo za Pembe ya Afrika zitaendelea kufanya kazi bega kwa bega ili kulitokomeza jinamizi la ugaidi.
Akiongea kuhusu shambulizi la hivi karibuni lililoua mamia ya watu, Desalegn amesema Addis Ababa haiwezi kuruhusu genge hilo la kitakfiri livuruge usalama, amani na uthabiti katika eneo hilo.
Waziri Mkuu wa Ethiopia amebainisha kuwa, lengo lake kuu kwa sasa ni kuhakikisha shambulio kama la Oktoba 14 halishuhudiwi tena, akisisitiza kuwa, nchi yake itaendelea kufanya jitihada za kuliangamiza genge hilo la kigaidi, kupitia jumuiya ya kieneo ya IGAD na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM.
Oktoba 14 watu zaidi ya 360 waliuawa katika hujuma za kigaidi zilizoulenga mji wa Mogadishu, huku mamia ya wengine wakiachwa na majeraha.
Kwa upande wake, Rais wa Somalia amesema kuna haja nchi zote za eneo kuimarisha juhudi za kuyasambaratisha magenge ya kigaidi, ambayo sio tishio tu kwa usalama na uthabiti wa nchi hiyo, bali kwa eneo zima la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.