Nov 26, 2017 13:17 UTC
  • Mapigano yaanza tena katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

Duru za habari zinaripoti kutoka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwamba, mapigano makali yamezuka tena katika nchi hiyo na kuzusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia.

Habari kutoka Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati zinasema kuwa, mapigano makali yamezuka kati ya waasi wa zamani wa SELEKA na kundi moja la wanamgambo kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Baadhi ya duru zinasema kuwa, mapigano hayo ni makali na kwamba, mamia ya raia tayari wamelazimika kuyahama makazi yao na kukimbilia katika kambi za wakimbizi zilizoko jirani na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA.

Mapigano hayo yamepelekea kuadimika bidhaa za chakula katika maeneo hayo ya kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, huku mashirika ya kimataifa ya utoaji misaada yakishindwa kuwafikia raia kwa ajili ya kuwapatia misaada.

Askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA

Hayo yanajiri katika hali ambayo ukosoaji dhidi ya wanajeshi hao wa MINUSCA wapatao elfu 13  umeendelea kuongezeka kutokana na wananchi kutoridhishwa na utendaji wa vikosi hivyo katika kuwalinda raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yalizuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya rais  Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi na magaidi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi. 

Tags