Dec 11, 2017 13:43 UTC
  • UN yaeleza wasiwasi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu Libya

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ameeleza wasiwasi wake kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanyika nchini humo.

Ghassan Salamé amesema kuwa, ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Libya umefikia kiwango cha kutia wasiwasi mkubwa na kwamba pande zote zinazopigana nchini humo haziwajibiki na wahusika wa uhalifu huo hawachukuliwi hatua yoyote.

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema kuwa, mamia ya raia wameuawa katika mapigano, milipuko na mashambulizi ya kikatili nchini Libya katika mwaka huu wa 2017 pekee.

Mabaki ya maiti za wawatu waliouawa katika machafuko ya ndani Libya

Ghassan Salamé ameongeza kuwa, Umoja wa Mataifa unawataka maafisa na wananchi wa Libya kufanya jitihada za kuboresha hali ya haki za binadamu na kwamba wawe na matumaini kuwa wanaungwa mkono na umoja huo.

Libya ilitumbukia katika machafuko ya ndani mwaka 2011 baada ya Marekani na washirika wake katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), kuivamia nchi hiyo.

Tags