Maandamano ya fujo yaendelea Tunisia; idadi ya waliokamatwa yafikia watu 600
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38835-maandamano_ya_fujo_yaendelea_tunisia_idadi_ya_waliokamatwa_yafikia_watu_600
Maafisa wa serikali ya Tunisia wametangaza kuwa idadi ya watu waliokamatwa katika maandamano ya fujo yaliyoendelea kwa usiku wa tatu hapo jana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kulalamikia ongezeko la bei za bidhaa na kodi imefikia watu 600.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jan 11, 2018 12:54 UTC
  • Maandamano ya fujo yaendelea Tunisia; idadi ya waliokamatwa yafikia watu 600

Maafisa wa serikali ya Tunisia wametangaza kuwa idadi ya watu waliokamatwa katika maandamano ya fujo yaliyoendelea kwa usiku wa tatu hapo jana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kulalamikia ongezeko la bei za bidhaa na kodi imefikia watu 600.

Hapo awali Khalifa Al-Shaibani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia alikuwa ametangaza kuwa askari polisi 49 walijeruhiwa na waandamanaji 206 walitiwa nguvuni siku ya Jumanne usiku katika maandamano ya upinzani yaliyofanyika katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Maafisa wa serikali ya Tunis aidha wametangaza kuwa vikosi vya usalama vimefanikiwa kudhibiti hali ya mambo katika mji wa Tebourba ulioko kwenye mkoa wa Manouba baada ya kupambana na waandamanaji.

Vikosi hivyo vilipelekwa pia katika mji wa Thala ulioko karibu na mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Algeria baada ya waandamanaji kuchoma moto jengo la taifa la usalama na kuwalazimisha polisi kuondoka katika mji huo.

Jeshi la Tunisia pia limetumwa katika miji kadhaa ukiwemo mji wa kitalii wa Soussse, Kebeli na Bizert kulinda majengo ya serikali ambayo yamekuwa yakilengwa na waandamanaji.

Vijana wakiandamana nchini Tunisia kulalamikia ongezeko la bei za bidhaa

Maandamano ya kupinga serikali nchini Tunisia kulalamikia ongezeko la bei za bidhaa na kodi yalianza tangu Jumatatu iliyopita.

Waziri Mkuu wa Tunisia Yussuf Shahid alitoa tamko hapo jana la kulaani vitendo vya hujuma na uharibifu vinavyofanywa katika maandamano hayo na kuelekeza kidole cha tuhuma kwa wapinzani kwamba wao ndio wanaobeba dhima ya vitendo hivyo.

Serikali ya Tunisia imeanza kutekeleza sera za kubana matumizi kiuchumi kutokana na kushuka mno thamani ya sarafu ya nchi hiyo na kukabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti.../