Upinzani Ethiopia wataka kufanyika mazungumzo ya kitaifa
(last modified Thu, 25 Jan 2018 03:00:30 GMT )
Jan 25, 2018 03:00 UTC
  • Upinzani Ethiopia wataka kufanyika mazungumzo ya kitaifa

Kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Ethiopia ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa kuhusu mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini humo.

Merera Gudina ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la AFP, siku chache baada ya kuachiwa huru. 

Amesema: "Njia pekee ya kuikomboa Ethiopia, ni kwa chama tawala kuitisha mdahalo wa kitaifa na vyama vya upinzani kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mzozo wa kisiasa unaoikabili nchi hii."

Merara Gudina, kiongozi wa chama cha upinzani cha Oromo Federalist Congress ambaye alikamatwa mwaka jana aliporejea kutoka Ulaya, wakati nchi hiyo ilikuwa chini ya sheria ya hali ya hatari amesema kuwa anaamini kwamba serikali alimtia mbaroni kwa shabaha ya kuzima malalamiko ya wapinzani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Makabiliano kati ya polisi na waandamanaji mjini Addis Ababa

Gudima aliachiwa huru hivi karibuni pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa wapatao 115. Watetezi wa haki za binadamu wanasema kuwa karibu wafungwa elfu mbili wa kisiasa wangali wanashikiliwa katika jela za Ethiopia.  

Siku chache zilizopita Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn alitangaza mpango wa serikali wa kufuta mashitaka dhidi ya wafungwa wote wa kisiasa sambamba na kufunga jela ya kuogofya ambako wafungwa hao walikuwa wanazuiliwa.