Kiongozi wa chama cha ANC: Afrika Kusini imeingia katika zama mpya
Kiongozi mpya wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha Kongresi ya Taifa (ANC ) amesema kuwa nchi hiyo imeingia katika zama mpya chini ya uongozi wake; hiyo ikiwa ni ishara mpya kwamba siku za Jacob Zuma kukalia kiti cha rais zinahesabika.
Matamshi hayo ya Cyril Ramaphosa yanabainisha wazi azma ya chama cha ANC ya kurejesha imani ya wawekezaji kwa chama hicho sambamba na kuwavutia wapiga kura kabla ya uchaguzi ujao kwamba kinaweza kuboresha uchumi wa Afrika Kusini. Matamshi hayo ya Mwenyekiti wa ANC pia ni ishara kuwa chama hicho kinataka kujisafisha na taswira ya ufisadi uliyokigubika tangu Zuma akalie kiti cha urais mwaka 2009.
Akizungumza pambizoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi huko Davos ambako ameuongoza ujumbe wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema: "Kwa sasa tupo katika zama mpya. Tulikuwa na uongozi wa zamani wa ANC na sasa tuna uongozi mpya wa chama. Viongozi wengi wa kibiashara niliokutana nao hapa wamesema kuwa wanatiwa moyo na mwelekeo wa sasa nchini Afrika Kusini".
Chama tawala nchini Afrika Kusini ANC kinajadili iwapo kutamlazimisha Rais Zuma kujiuzulu kiti cha urais kabla ya kumalizika muhula wake wa pili wa uongozi au la.