Afisa wa ngazi ya juu wa ANC: Zuma anapasa kujiuzulu
Afisa wa ngazi ya juu katika chama tawala nchini Afrika Kusini (ANC) amesema kuwa Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo anapasa kujiuzulu na hivyo kuzidisha mashinikizo kwa Zuma ambaye anaonekana kudhoofika tangu Cyril Ramaphosa achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa chama tawala ANC mwezi Disemba mwaka jana.
Mashinikizo na miito inayomtaka Zuma ajiuzulu yamekuwa yakiongezeka siku baada ya siku; ambapo wiki hii Rais huyo wa Afrika Kusini anatazamia kukutana na maafisa sita wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho tawala. Cyril Ramaphosa ana nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi ujao wa rais nchini Afrika kusini huku idadi kubwa ya wanachama wakimtaka Zuma ajiuzulu ili kutoa nafasi kwa Ramaphosa ya kutekeleza ajenda yake ya mapambano dhidi ya ufisadi.
Mweka hazina mkuu wa chama cha ANC Paul Mashatile ameeleza kuwa kunapasa kuwepo mabadiliko ya usimamizi na kwamba haiwezekani chama hicho kikawa na vituo viwili vya madaraka. Amesema njia bora zaidi ya kufanikisha suala hilo ni kwa Rais kuondoka madarakani.
Zuma ambaye anakabiliwa na tuhuma za ufisadi amekuwa katika nafasi yenye kulegalega tangu nafasi yake na mkuu wa chama tawala ANC ichukuliwe na Makamu wa Rais, Cyril Ramaphosa.