Mwenyekiti wa ANC akanusha uvumi wa kupatiwa Rais Zuma kinga ya kutoshtakiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i40173-mwenyekiti_wa_anc_akanusha_uvumi_wa_kupatiwa_rais_zuma_kinga_ya_kutoshtakiwa
Mwenyekiti wa Chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC amekanusha taarifa za kupatiwa kinga ya kutoshtakiwa Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2018 04:21 UTC
  • Mwenyekiti wa ANC akanusha uvumi wa kupatiwa Rais Zuma kinga ya kutoshtakiwa

Mwenyekiti wa Chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC amekanusha taarifa za kupatiwa kinga ya kutoshtakiwa Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo.

Cyril Ramaphosa amesema hayo katika hotuba yake mbele ya wajumbe wa chama cha ANC Bungeni na kukanusha tetesi za kupatiwa kinga ya kutoshtakiwa Rais Jacob Zuma.

Tetesi hizo zimezuka baada ya kufanyika mazungumzo baina ya Cyril Ramaphosa na Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo yaliyokuwa na lengo la kujadili kujiuzulu Zuma.

Licha ya Ramaphosa kutangaza kwamba, natija ya mazungumzo hayo itatangazwa hivi karibuni, lakini baadhi ya duru zimefichua kwamba, Rais Zuma amekubali kujiuzulu kwa masharti.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini anayeandamwa na mashinikizo ili ajiuzulu

Duru hizo zinasema kuwa, miongoni mwa masharti hayo ni kupatiwa kinga ya kutoshtakiwa.

Ramaphosa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini amesema, mazungumzo yake na Jacob Zuma yalikuwa mazuri na yamechunguza njia bora na za haraka za kutatua matatizo ya nchi hiyo. Rais Jacob Zuma amezidi kuwa chini ya mashinikizo ya chama tawala cha ANC tangu Cyril Ramaphosa alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho. Iwapo Jacob Zuma atajiuzulu, Cyril Ramaphosa ambaye ni makamu wake atachukua uongozi wa Afrika Kusini hadi utakapoitishwa uchaguzi mwingine wa rais mwaka 2019.

Jacob Zuma amekuwa madarakani tangu mwaka 2009 na katika miaka ya hivi karibuni Rais huyo wa Afrika Kusini amekuwa akiandamwa na kashfa kadhaa za ufisadi.