Mazungumzo kuhusu hatima ya Rais Zuma yanaendelea nchini Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i40233-mazungumzo_kuhusu_hatima_ya_rais_zuma_yanaendelea_nchini_afrika_kusini
Mazungumzo kuhusu hatima ya Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini yanaendelea huku duru za karibu na mazungumzo hayo zikisema kwamba, kuna masuala mbalimbali yanayojadiliwa katika mazungumzo hayo lakini ajenda kuu ni kuhusu suala la kujiuzulu Zuma.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 11, 2018 11:37 UTC
  • Mazungumzo kuhusu hatima ya Rais Zuma yanaendelea nchini Afrika Kusini

Mazungumzo kuhusu hatima ya Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini yanaendelea huku duru za karibu na mazungumzo hayo zikisema kwamba, kuna masuala mbalimbali yanayojadiliwa katika mazungumzo hayo lakini ajenda kuu ni kuhusu suala la kujiuzulu Zuma.

Cyril Ramaphosa, Mwenyekiti wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC amesema kuwa, amekutana tena na kufanya mazungumzo na Rais Zuma na kwamba, ajenda kuu ni suala la Zuma kujiuzulu na kukabidhi uongozi kutokana na mashinikizo dhidi yake.

Hata hivyo baadhi ya duru zinasema kuwa, Rais Zuma ametangaza kuwa yuko tayari kujiuzulu lakini ametoa masharti; na sharti kuu ni kupatiwa kinga ya kutoshtakiwa.

Akizungumzia sharti hilo, Mwenyekiti wa Chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC amekanusha taarifa za kupatiwa kinga ya kutoshtakiwa Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

Ramaphosa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini amenukuliwa akisema kuwa, mazungumzo yake na Jacob Zuma yanaendelea vizuri na yamechunguza njia bora na za haraka za kutatua matatizo ya nchi hiyo. Rais Jacob Zuma amezidi kuwa chini ya mashinikizo ya chama tawala cha ANC tangu Cyril Ramaphosa alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho. Iwapo Jacob Zuma atajiuzulu, Cyril Ramaphosa ambaye ni makamu wake atachukua uongozi wa Afrika Kusini hadi utakapoitishwa uchaguzi mwingine wa rais mwaka 2019.

Jacob Zuma amekuwa madarakani tangu mwaka 2009 na katika miaka ya hivi karibuni Rais huyo wa Afrika Kusini ameandamwa na kashfa kadhaa za ufisadi.