Ramaphosa aahidi kutomvumilia fisadi yoyote Afrika Kusini
Mwenyekiti Taifa wa chama tawala cha ANC cha Afrika Kusini ameahidi kupambana vikali na mafisadi na kutomvumilia mbadhirifu yeyote wa mali ya umma.
Cyril Ramaphosa amesema hayo baada ya mazungumzo yake na Rais Jacob Zuma jana Jumapili akisisitiza kuwa, watuhumiwa wote wa ubadhirifu wa fedha za umma watapandishwa kizimbani huko Afrika Kusini.
Aidha amekiri kuwa chama cha ANC kiko katika hatari ya kugawanyika lakini pamoja na hayo kitaendelea na vita vyake dhidi ya ufisadi.
Matamshi hayo ya Ramaphosa yametolewa katika hali ambayo Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini anatuhumiwa kufanya ufisadi wa kila aina wa fedha za umma kiasi kwamba hata wanachama wenzake ndani ya ANC wanamshinikiza ajiuzulu kabla ya kumalizika kipindi chake cha urais hapo mwakani.
Rais Jacob Zuma amezidi kuwa chini ya mashinikizo ya chama tawala cha ANC tangu Cyril Ramaphosa alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho. Hivi sasa ANC imegawika baina ya waungaji mkono wa Zuma na wapinzani wake na hadi sasa imeshindwa kumlazimisha Jacob Zuma ajiuzulu kabla ya kumalizika kipindi chake cha urais mwakani.
Iwapo Jacob Zuma atajiuzulu, Cyril Ramaphosa ambaye ni makamu wake atachukua uongozi wa Afrika Kusini hadi utakapoitishwa uchaguzi mwingine wa rais mwaka 2019.