Feb 13, 2018 08:10 UTC
  • Msemaji wa waasi wa Sudan Kusini ahukumiwa kifo

Msemaji wa waasi nchini Sudan Kusini, James Gatdet Dak amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya uhaini.

Jaji Ladu Armenio wa mahakama moja mjini Juba hapo jana alimpata Gatdet Dak na hatia ya uhaini na jinai nyingine dhidi ya dola na kumhukumu kifo kwa kunyongwa.

Hukumu hiyo imetolewa takriban mwaka mmoja baada ya msemaji huyo wa waasi kurejeshwa kwa nguvu nchini Sudan Kusini akitokea Kenya, licha ya kusajiliwa kama mkimbizi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Dak ambaye ni mwandishi wa habari wa zamani licha ya kukanusha mashtaka yote dhidi yake, lakini amehukumiwa kifungo cha miaka 21 jela kwa kupatikana na hatia ya mashitaka mbali mbali yaliyokuwa yakimuandama, na anatazamiwa kutuhukia kifungo hicho kabla ya hukumu yake ya kunyongwa kutekelezwa.

Genge la waasi nchini Sudan Kusini

Haya yanajiri katika hali ambayo, mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika yanaendelea katika nchi jirani ya Ethiopia, licha ya vikosi vya waasi na serikali kuelekezeana kidole cha lawama kuhusu mapigano yanayoendelea.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.

Tags