Waziri Mkuu wa Ethiopia ajiuzulu baada ya machafuko ya ndani
Waziri Mkuu wa Ethiopia amejiuzulu nyadhifa zake zote mbili kama waziri mkuu na Mwenyekiti wa chama tawala.
Uamuzi wa Hailemariam Desalegn wa kujiuzulu umechukuliwa kufuatia mlolongo wa migogoro ya kisiasa na machafuko ya mara kwa mara katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Wiki kadhaa zilizopita Hailemariam Desalegn alijaribu kupunguza migogoro ya kisiasa iliyokuwa imemzonga kwa kuwaachia huru maelfu ya wafungwa wakiwemo wafungwa wa kisiasa.
Mamia ya watu wamepoteza maisha nchini Ethiopia katika ghasia na machafuko ya ndani yaliyopamba moto zaidi mwaka 2015 na 2016 kutokana na malalamiko ya watu wa makabila ya Oromo na Amhara.
Askari usalama wa serikali ya Ethiopia wamekamata makumi ya maelfu ya watu na kuua waandamanaji zaidi ya 900 tangu yalipoanza maandamano ya watu wa Oromo waliokuwa wakipinga unyakuzi wa ardhi zao, ukandamizaji wa kisiasa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na vyombo vya dola.

Akihutubia taifa hii leo kabla ya kujiuzulu, Hailemariam Desalegn amesema machafuko na migogoro ya kisiasa imesababisha kupoteza maisha na makazi watu wengi na kwamba kujiuzulu kwake ni hatua muhimu kwa jitihada za kufanya mageuzi ambayo yataielekeza nchi kwenye amani endelevu na demokrasia.
Hjata hivyo amesisitiza kuwa ataendelea kuongoza kama Waziri Mkuu hadi pale chama tawala cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF) na Bunge la nchi hiyo litakapomchagua waziri mkuu mpya.