Ramaphosa achaguliwa kuwa Rais mpya wa Afrika Kusini
Bunge la Afrika Kusini limemchagua Cyril Ramaphosa ambaye ni Mwenyekityi wa chama tawala cha ANC kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
Hatua hiyo imechukuliwa na Bunge la Afrika Kusini baada ya kujiuzulu rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma.
Bunge la Afrika Kusini lenye wabunge 400 ambalo linadhibitiwa na chama cha ANC, limemchagua Ramaphosa hii leo kukamilisha kipindi cha uongozi wa Zuma kitakachomalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka kesho wa 2019.
Jacob Zuma mwenye umri wa miaka 75 alilazimika kujiuzu jana Jumatano kutokana na mashinikizo ya chama chake cha ANC kilichukuwa kimempa masaa 48 kung'atuka madarakani.
Disemba mwaka jana kiongozi mpya wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye ana umri wa miaka 65 alimpiku kwa kura chache sana Nkosazana Dlamini-Zuma katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya mwenyekiti wa chama tawala cha ANC.
Ramaphosa ambaye alifungwa mara kadhaa nchini Afrika kutokana na harakati zake za kupigania ukombozi, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa ANC mwaka wa 1991, na katika miaka iliyofuata alikuwa na nafasi muhimu katika mazungumzo ya kuelekea kwenye utawala wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini kwa niaba ya chama cha ANC.
Baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia alichaguliwa kuwa mbunge na kushiriki katika utungaji wa katiba mpya ya nchi hiyo. Wakati huo alichukuliwa kama naibu wa Nelson Mandela, rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, lakini alipoteza nafasi hiyo kwa Thabo Mbeki, aliyekuwa rais wa nchi mwaka 1999.
Baadaye Cyril Ramaphosa alijihusisha na biashara hususan katika sekta ya madini na kilimo na hii leo anatambulika kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa zaidi nchini Afrika Kusini.